Bondia raia wa Urusi, Maxim Dadashev ameaga dunia baada ya pambano lake na Subriel Matias kumsababishia majeraha makubwa kwenye ubongo.
Bondia huyo mwenye umri wa miaka 28, katika raundi ya 11 ya pambano lililopigwa mwishoni mwa wiki iliyopita, alipokea kichapo kikali bila majibu na kushindwa kutembea mwenyewe hali iliyopelekea mkufunzi wake Buddy Mc Girt kulazimisha pambano lisimamishwe.
Punde tu baada ya pambano bondia Dadashev alikimbizwa hospitali ambapo madaktari waligundua kuwa damu ilikuwa imevuja kwenye ubongo na kufanyiwa upasuaji wa haraka lakini juhudi za madaktari hazikufua dafu, ambapo jana jumanne alifariki.
kwamujibu wa taarifa zilizotolewa na shirikisho la ngumi la Urusi limesema kuwa tayari uchunguzi umeshafunguliwa juu ya mkasa huo huku katibu mkuu wa shirikisho hilo, Umar Kremlev akiwa na shaka juu ya uvunjwaji wa taratibu katika pambano hilo.
“Kulikuwa na aina fulani ya uvunjwaji wa taratibu, tumempoteza Maximu Dadashev ilikuwa ni nyota yetu inayochipua,” amesema Kremlev
Aidha, amesema licha ya kuwa na tatizo kama hilo linaweza kutokea kwenye mchezo wowote anaamini kuna mapungufu ya kibinadamu yamechangia na ameahidi kuunga mkono familia ya marehemu ikiwemo kifedha na kuafuatilia uchunguzi hadi kujua ukweli.
Bondia Dadashev alikuwa akifanya shughuli zake za masumbwi nchini Marekani na alikuwa anashanda mapambano yake yote 13 aliyocheza kabla ya pambano la ijumaa alilo pambana na Matias kutoka Puerto Rico ambapo alipigwa makonde mazito kwa kasi kali iliyopelekea mauti yake.
Kwa upande wa mkufunzi wake, Mc Girt ameeleza vyombo vya habari nchini humo kuwa alishindwa kumshawishi mwanafunzi wake kukubali kushindwa, lakini alipoona anazidiwa aliamua kurusha taulo ulingoni ili kusimamisha pambano.