Bondia Benson Mwakyembe amefanikiwa kushinda pambano lake dhidi ya Mada Maugo katika mchezo uliopigwa usiku wa kuamkia leo mjini Songea kutokana na mpinzani wake kuvunja sheria za mchezo huo.
Mchezo huo ambao ulikuwa ukisubiriwa kwa hamu kubwa na wakazi wa Songea, ulikuwa na upinzani mkali ambapo mkongwe Maugo alionyesha ufundi wa hali ya juu wa kurusha makonde kwa mpinzani wake.
Katika Raundi ya sita mkongwe Maugo alimwangusha Mwakyembe mara mbili kitu kilichoashiria kuwa mchezo huo ungeweza kumalizika kwa ‘KO’.
Lakini hali ilikuwa kinyume pale Maugo alipomshambulia mpinzani wake akiwa amelala chini kitu ambacho ni kosa kwa mujibu wa sheria zinazoongoza mchezo huo.
Kutokana na kitendo hicho majaji wote watatu waliamua kumpa ushindi Mwakyembe ambaye kimsingi alishapoteza mchezo huo.
Katika mchezo wa utangulizi ‘Mfalme wa Wazaramo’ Abdalah Pazi aliendeleza rekodi ya kushinda katika raundi ya kwanza baada ya kumpiga Fransic Mwamasu huku bondia Man Chuga akimsambaratisha Mussa Chipepeta kwa pointi na kufanya timu iliyotoka jijini Dar es salaam kurudi kidedea.
Wakati huo huo Rais wa Chama cha ngumi nchini Chaurembo Palasa ametoa onyo kali kwa mabondia wote nchini watakaofanya vitendo vya utovu wa nidhamu wawapo uwanjani.
Palasa ameyasema hayo baada ya mchezo uliomkutanisha Stam Kessy na Twaha Kiduku kuisha kwa Kessy kugomea matokeo akidai sio ya kweli.
“Bondia yoyote atakayefanya utovu wa nidhamu ulingoni atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za ngumi ili kukomesha vitendo hivi,” alisema Palasa.
Kessy alifanya fujo kwenye meza ya Majaji hali iliyoonyesha utovu mkubwa wa nidhamu kwenye ukumbi wa Vijana Kinondoni juzi Jumapili.