SHABIKI wa timu ya Tanzania Taifa Stars Bongo Zozo, amempongeza Kocha Mkuu wa timu hiyo Kim Poulsen, kufuatia ushindi wa mabao 3-2 uliopatikana jana Jumanne (Septemba 07), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Bongo Zozo ambaye ni Raia wa England, amekua shabiki mkubwa wa timu ya taifa ya Tanzania kwa siku za hivi karibuni, huku wadau wengi wa soka nchini wakivutiwa na namna anavyoongea vizuri lugha ya kiswahili.
Akizungumza na Dar24 Media baada ya mchezo huo, Bongo Zozo alisema amefurahi kuona wachezaji wa Taifa Stars walivyofuata maelekezo ya Kocha Kim Poulsen, na kufikai hatua ya kupambana kwa nguvu katika kipindi cha pili cha mchezo.
alisema Kocha Paolsen alifanya kazi kubwa ya kuwaelekeza wachezaji wake wakati wa mapumziko, na jambo hilo lililonekana uwanjani katika kipindi cha pili ambapo Taifa Stars walipata bao la ushindi na kuufanya mchezo kumalizika kwa mabao 3-2, wakiwa katika Uwanja wa nyumbani.
“Katika kipindi cha pili wachezaji wa Taifa Stars walionesha kiwango bora na kufanikiwa kuwashinda kirahisi wapinzani wetu ambao walionesha kuzinduka dakika za mwisho za kipindi cha kwanza baada ya kusawazisha mabao mawili.”
”Kipindi cha kwanza wachezaji wa Taifa Stars hawalikua vizuri sana, hili lilitukatisha tamaa sisi mashabiki tuliokua tunafuatilia mchezo huu, na kujua huenda tungefungwa.”
”Katika kipindi cha pili, Taifa Stars walionesha uwezo mkubwa wa kupambana kwa kasi na kumshambulia upande wa wapinzani wao na mwisho wa mchezo tukashinda.” alisema Bongo Zozo.
Ushindi wa mabao 3-2 unaiwezesha Taifa Stars kuongoza msimamo wa kundi J, lenye timu za Benin, DR Congo na Madagascar.
Taifa Stars imefikisha alama 4 sawa na Benin baada ya kucheza michezo miwili dhidi ya DR Congo uliomalizika kwa sare ya 1-1 na Madagascar uliomalizika kwa ushindi wa mabao 3-2.