Boomplay App inayotoa huduma ya kusikiliza na kupakua muziki barani Afrika, imesaini makubaliano ya kushirikiana kibiashara na Warner Music, kwa lengo la kuongeza wigo wa upatikanaji wa kazi za muziki wa kampuni hiyo maeneo mengi zaidi duniani.

Moja kati ya makubaliano hayo ni pamoja na kuipa fursa Boomplay, kusambaza kazi za muziki zaidi ya milioni moja kutoka Warner Music kwenda kwa watumiaji wake nchini Tanzania na mataifa mengine tisa ya Kiafrika ikiwemo Cameroon, Ivory Coast, Ghana, Kenya, Nigeria, Rwanda, Senegal, Uganda na Zambia.

Ushirikiano huo utawawezesha wasanii wa Warner Music kujitangaza zaidi kwa haraka mbele ya mamilioni ya watumiaji wa Boomplay na kuiwezesha App hiyo kufikia dhamira yake ya kukusanya kazi za muziki kutoka sehemu mbali mbali za dunia na kuzileta barani Afrika.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Boomplay, Joe He amesema kuwa makubaliano hayo ya makampuni makubwa ya muziki ya kimataifa kama Warner Music, yanawawezesha kuyakaribia mafanikio ya malengo yao ya kujenga jukwaa kubwa la muziki linaloaminika na wengi barani Afrika.

“Tunataka kila mpenda muziki awe na uwezo wa kupata nyimbo na video, wakati wowote na mahali popote. tunatarajia uwepo wa mafanikio bora kupitia ushirikiano huu na muendelezo mzuri wa kibiasha tukiwa na Warner Music hasa katika kipindi hiki kizuri kwenye fani ya muziki Afrika,”amesema He.

Kwa upande wake, Meneja wa Boomplay Tanzania, Natasha Stambuli amesema kuwa wanatarajia mafanikio makubwa na fursa mbalimbali yakiwa ni matokeo ya makubaliano kama hayo katika tasnia ya muziki nchini Tanzania.

Naye Alfonso Perez Soto, ambaye ni Makamu wa rais wa Warner Music Ulaya Mashariki, Mashariki ya Kati na Afrika amebainisha kwamba wanafuraha kushirikiana na Boomplay kuleta kazi kutoka kwa wasanii kwa mamilioni ya wasikiliza na wapenzi wa muziki barani Afrika.

Tangu mwaka uliopita, Boomplay imeendelea kutikisa anga la muziki kwa kutangaza ushirikiano na makampuni mbali mbali makubwa ili kupata watumiaji wengi zaidi kila mwezi na kutoa version (toleo) ya iOS mwezi Disemba mwaka 2018.

 

Mr Beneficial: Yale ni maisha nimewahi kuyaishi Arusha
Wananchi waonywa kutumia vibaya jina la JPM