Chama cha ACT – Wazalendo kimeeleza kusikitishwa na kauli za mgombea Urais wa Tanzania kupitia chama hicho Bernad Membe, jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuwa yeye ni mgombea halali wa chama hicho.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Chama cha ACT- Wazalendo Taifa na mgombea urais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu mchakato wa kampeni za chama hicho na suala la upigaji kura.
“Membe alipokuja tulimwambia uamuzi wa mkutano mkuu ni tushirikiane na vyama vingine, tukamuuliza tukiamua kushirikiana utakubali, akasema “Naam”, tulipoona kampeni zetu zimesuasua, tukaamua, na Membe akiwepo, tumuunge mkono Tundu] Lissu.” amesema Maalim Seif.
“Mgombea wetu (Bernard Membe), haonekani. Ni afadhali mzee wa ubwabwa (Hashim Rungwe) anaonekana. Kamati ya uongozi kwa kauli moja pamoja na Membe tulikubaliana tumuunge mkono Tundu Lissu.” ameongeza Maalim Seif
Jana Oktoba 19, Membe aliitisha mkutano na waandishi wa habari ambapo alieleza kuwa yeye bado ni mgombea halali wa Chama hicho na Oktoba 28 mwaka huu ataipeleka ACT – Wazalendo ikulu.