Waziri Mkuu wa zamani Boris Johnson amejiondoa kwenye kinyang’anyiro cha uwaziri mkuu, ikiwa ni wiki chache tu baada ya kushindwa katika azma yake ya kukiongoza chama Conservative Part.
hatua hiyo imemuacha Rishi Sunak akipigiwa upatu kuchaguliwa kwenye wadhifa huo na huenda hali itabadilika kwa Sunak na kutangazwa mkuu wa chama hicho leo, hasa baada ya Boris Johnson aliyetizamwa kuwa mshindani wake mkuu kutangaza kujiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho usiku wa kuamkia leo.
Mshindi anahitajika kuungwa mkono na wabunge wasiopungua 100 wa chama cha Conservative kwa njia ya kura. Shughuli hiyo ya kupiga kura imepangwa kufanyika leo mchana.
Inaelezwa kuwa mpaka October 21, 2022, Sunak tayari alikuwa anaungwa mkono na takriban wabunge 150 wa chama hicho.
Hatua ya Boris Johnson kutangaza kujiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho hata kabla atangaze rasmi kuwa angewania, imemuacha waziri Penny Mordaunt kuwa mshindani pekee wa Sunak.
Hata hivyo Mordaunt hajapata uungwaji mkono mkubwa miongoni mwa wabunge wa chama chake.
Anatarajiwa kukabiliwa na shinikizo kubwa kuachana na azma hiyo ili kukamilisha shughuli ya kumpata waziri mkuu mpya mapema, mnamo wakati Uingereza ikikabiliwa na migogoro kadhaa.
Ikiwa Mordaunt mwenye umri wa miaka 49 atakataa kuachana na azma yake, na aweze kupata kura 100, basi uamuzi utafanywa na wanachama 170,000 wa Conservative kwa kupiga kura baadaye wiki hii mtandaoni na matokeo kutangazwa Ijumaa.
Miezi miwili iliyopita, wanachama walimchagua Truss aliyemshinda Sunak, licha kwamba Sunak alikuwa na uungwaji mkono wa wabunge wengi wa Conservative kuliko Truss.
Hatua ya kwanza kwenye kinyang’anyiro hicho ni jumla ya wabunge 357 wa Conservative kupiga kura ya ishara alasiri ya leo kuonesha ni mgombea yupi anaungwa mkono zaidi katika chama hicho ambacho kwa sasa kimegawika.
Hii ni mara ya pili ndani ya miezi miwili kwa chama cha Conservative kumchagua waziri waziri mkuu mpya ndani ya miezi miwili.
Liz Truss aliyekuwa amehudumu kwa siku 44 pekee, alijiuzulu wiki iliyopita baada ya mpango wake wa punguzo la kodi kuzusha mtikisiko katika masoko ya fedha.
Truss alichukua usukani mapema mwezi Septemba kutoka kwa Boris Johnson ambaye pia alilazimika kujiuzulu kufuatia kashfa ya sherehe iliyoandaliwa wakati wa vikwazo vya kudhibiti virusi vya corona na vilevile kwa kulidanganya bunge kuhusu sherehe hiyo.
Wakosoaji wakuu ndani ya chama hicho walitahadharisha kwamba kungeshuhudiwa wimbi la wabunge wake kujiuzulu endapo Johnson angerejea tena kuwa waziri mkuu, hali ambayo ingesababisha uchaguzi mkuu unaoitishwa na vyama vya upinzani kuandaliwa.
Utafiti wa maoni uliofanywa mwishoni mwa wiki ulidokeza kuwa huenda chama cha Conservative kikanufaika kubadilisha kiongozi wao baada ya hatua za Truss kuwashusha chini kisiasa.