Mvua zinazoendelea kunyesha nchini, zimesababisha mafuriko ambayo yamekata mawasiliano ya ndani wilayani Rufiji mkoa wa Pwani zikiwemo barabara mbalimbali za wilaya hiyo ikiwemo inayotoka kibiti kwenda katika eneo la mradi wa umeem (MW 2,115) katika maporomoko ya mto rufiji na kuziacha kaya zaidi ya 350 bila makazi.
Aidha baadhi ya barabara zinazounganisha kata 13 za Rufiji hazipitiki kutokana na makaravati kusombwana maji na daraja la Ikwiriri limeonyesha dalili za kubomoka hali inayotishia kukatika kwa mawasiliano na mikoa ya kusini.
Mbunge wa wa Rufiji (CCM) Mohamed Mchengerwa amesema msaada unaohitajika wa haraka katika wilaya ya Rufiji ni chakula na mbegu ili kuwawezesha wakulima kupanda mazao ya muda mfupi kuepuka njaa inayoweza kuwakumba.
Amesema kuwa mara baada ya mafuriko kaya zilizokumbwa na maafa zilihamishiwa shule ya Msingi Mhoro na majengo ya serikali ya chumvi lakini baadaye eneo hilo pia lilijaa maji huku kukiwa na tatizo la chakula hivyo wananchi hao wakaombwa kwenda kwa ndugu zao.
”Pale tulishindwa kuwahudumia kwakuwa chakula mahitaji mengine havikuwepo ndipo tukawaomba watafute sehemu pa kwenda yaani hatujui wanaishi wapi kwa sasa” amesema Mchengerwa
Hata hivyo Mbunge huyo ameiomba Serikali kuwapa misaada mbalimbali wananchi wake kwasababu hawana huduma zozote na ili watoke eneo moja kwenda eneo jingine wanahitajika kupanda boti au mitumbwi ambayo gharama yake sh 5000 kiwango ambacho amesema hawawezi kuimudu.
Naye mkurugenzi wa kitengo cha maafa Ofisi ya Waziri mkuu Kanali Jimmy Matamwe amesema baada ya kupokea taarifa hiyo amefika rufiji na kutoa msaada wa boti mbili na wazamiaji ili kuwaokoa wananchi waliokuwa wamezingirwa na maji.
Mkuu wa mkoa wa pwani Evarest Ndikilo amesema rufiji imeathirika zaidi kwa kuwa inapokea maji kutoka mito ya Kilombelo Ruaha Mkuu na Ruengu inayokutanisha bwawa la Nyerere na kwamba mabwawa ya mtera na kidatu yamejaa.