Rais Samia Suluhu Hassan amesema benki za biashara zinatarajia kushusha riba ya mikopo zinazotoa kwa wananchi baada ya majadiliano yaliyodumu kwa miezi kadhaa.
Rais Samia amesema hayo leo Novemba 25 alipofungua mkutano wa 20 wa taasisi za fedha nchini ulioandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ikiwa imepita miezi mitano tangu alipoiagiza benki hiyo kuangalia namna ya kuwapunguzia wananchi maumivu ya marejesho.
“Leo nafurahishwa na kauli niliyoisikia hapa kwamba Benki Kuu wamelifanyia kazi suala hili na tumemsikia mwenyekiti wa wakurugenzi wa benki Tanzania kwamba hivi tutasikia wakitangaza kushusha riba ya mikopo kwa sekta binafsi,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema amegundua ukuaji wa sekta binafsi hauendi vizuri kutokana na mikopo kutoelekezwa zaidi katika sekta hiyo inayoajiri watu wengi zaidi nchini.
Mapema Juni, alipokuwa akizindua jengo la BoT jijini Mwanza, Rais Samia aliiagiza benki hiyo kushughulikia changamoto zote zinazofanya riba iwe juu ili ishuke mpaka chini ya asilimia 10.
Gavana wa BoT, Profesa Florens Luoga amesema mkutano huo umekuwa jukwaa muhimu kwa wakuu wa taasisi za fedha, wasomi na watendaji kujadili maendeleo ya sekta ya benki na fedha pamoja na uchumi kwa ujumla.
Katika kipindi cha miongo minne iliyopita, Profesa Luoga amesema wamefanya mikutano 19 kujadili masuala mbalimbali ambayo yaliakisi mahitaji ya wakati husika.
“Katika mkutano wa mwaka huu tunaufanya katikati ya janga la Uviko-19 kujadili namna ya kuimarisha uchumi na nchi inavyoweza kuimarika na matumizi ya teknolojia,” amesema Gavana Luoga.
Awali, Mwenyekiti wa TBA, Abdulmajid Nsekela alisema BoT imefanya maboresho ya sera yatakayoongeza chachu ya kuzishawishi benki kupunguza riba.
Nsekela ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa Benki ya CRDB, amesema hadi sasa benki zimekuwa zikijiandaa kupunguza riba na kubainisha kuwa hivi karibuni moja baada ya nyingine zitaanza kutangaza punguzo hilo.
Katika Mkutano huo mambo manne yatajadiliwa ikiwamo ukuaji endelevu wa uchumi wakati na baada ya janga la Uviko-19, vipaumbele na sera mbadala, kuchochea kasi ya maendeleo ya kidijitali katika kuimarisha ukuaji endelevu wa uchumi ikiwa ni pamoja na sarafu za kidigitali, uzoefu, vihatarishi na usimamizi na kuongeza mikopo kwa sekta binafsi baada ya Uviko 19, wajibu wa Serikali, taasisi za fedha na sekta binafsi.