Klabu ya Manchester United imemfuta kazi aliyekuwa kocha wake, Jose Mourinho ikiwa ni siku mbili baada ya kipigo walichokipata dhidi ya klabu ya Liverpool Jumapili iliyopita.
Mourinho amefungashiwa vilago na kukamilisha safari yake ndani ya wekundu hao wa Old Trafford, safari aliyoianza Mei mwaka 2016 alipojiunga na timu hiyo akitokea Chelsea.
Man United wamekuwa katika wakati mgumu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Uingereza, ikiwa nyuma kwa alama 19 dhidi ya Liverpool ambayo imejikita katika kilele cha Ligi hiyo inayotajwa kuwa maarufu zaidi duniani.
Klabu hiyo imekuwa ikipata tabu hata kujiweka katika nafasi nne za juu kwenye Ligi hiyo, huku wachezaji wengi wakitajwa kuwa kwenye mgogoro mzito na meneja huyo mwenye utajiri wa maneno na tambo.
Mourinho alikuwa kwenye mvutano na Paul Pogba, Romelu Lukaku na Alexis Sánchez ambao ni wachezaji tegemezi wa klabu hiyo.
Hata hivyo, kocha huyo amekuwa akijitetea kuwa alishindwa kuingia kwenye Ligi na kikosi cha timu alichokuwa anakitaka kutokana na mwajiri wake kutoyapokea na kuyafanyia kazi mapendekezo ya kusajili wachezaji aliowapendekeza.
Kitendawili cha Mourinho ndani ya Man United kimetatuliwa rasmi, lakini fumbo la nani atamrithi linabaki katika muda huu.