Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Wa Baraza la Vijana Chadema (BAVICHA), Gertrude Ndibalema amehamia rasmi Chama cha Mapinduzi (CCM) na kukabidhiwa kadi ya uanachama.

Gertrude alikuwa ndani ya Chadema kwa miaka 8 tokea alipokuwa mwanafunzi wa chuo kikuu cha Dodoma (UDOM), kabla ya kuhamia rasmi CCM kwa madai kuwa ameamua kuingia chama kinacholea vijana na kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano ili kuendeleza ndoto zake.

Mbali na misukosuko aliyoeleza kuwa alipitia alipokuwa Chadema kama kusimamishwa chuo, amesema kuwa hakupata walicho ahidiwa na chama hicho, jambo lililochochea yeye kuhamia CCM.

Aidha, Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM, Mussa Mwakitinya alipokuwa akimkabidhi kadi ya CCM amesema kuwa uamuzi alioufanya ni sahihi na atarajie kupata ushirikiano mkubwa kuendeleza shughuli za maendeleo nchini.

Gertrude Ndibalema alijiuzulu u-Naibu Katibu Mkuu Wa Baraza la Vijana Chadema Machi 11, 2018 akidai anabaki kuwa mwanachama ili kutimiza majukumu yake binafsi.
Alipotangaza kujiuzulu alisema kuwa, “Kwa kuwa nakipenda chama changu na kwa taaluma yangu (mawasiliano kwa umma) ili kuepuka mgongano, nimeamua kukaa pembeni ili kutimiza azma yangu na nitabaki kuwa mwanachama.”
Gertrude alishika wadhifa huo tangu mwaka 2014 hadi alipotangaza kujiuzulu kupitia taarifa kwa umma, akiwa kiongozi wa pili wa ngazi ya juu Bavicha kujizulu ambapo alitanguliwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza hilo, Patrobas Katambi ambaye pia alijiunga na CCM na kuchaguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma.

 

Hizi hapa nafasi za ajira kutoka makampuni 10 Tanzania
Video: Waziri Mpina azindua mafunzo kwa wavuvi, awatangazia neema wanaokula samaki