Mahakama ya juu nchini Kenya imebatilisha uchaguzi wa urais nchini humo baada ya kujiridhisha kuwa ulikuwa na kasoro nyingi zilizokiuka katiba na utawala wa sheria.
Mahakama hiyo imesema kuwa imeridhishwa na ushahidi uliowasilishwa na upande wa walalamikaji ambao ni kambi ya NASA iliyokuwa imemsimamisha mgombea wake Raila Odinga, hivyo imeamuru uchaguzi huo kufanyika upya.
Kati ya majaji saba waliosikiliza kesi hiyo, majaji watano wameeleza kukubaliana na ushahidi wa upande wa walalamikaji kuwa kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa sheria katika uchaguzi huo uliofanyika Agosti 8 mwaka huu.
“Mlalamikiwa namba moja (Tume Huru ya Uchaguzi) ilishindwa, ilipuuzia na ilikataa kuendesha uchaguzi kwa misingi iliyoainishwa kwenye katiba,” hukumu hiyo imeeleza.
Imeeleza kuwa ukiukwaji mkubwa wa katiba na udanganyifu ulifanyika wakati wa kuhamisha na kujumlisha kura kwa njia ya kielektroniki.
Kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo, uchaguzi huo unapaswa kurudiwa ndani ya siku 60 tangu uamuzi wa mahakama kutolewa.
Tume Huru ya Uchaguzi ya Kenya ilimtangaza Uhuru Kenyatta kuwa mshindi wa uchaguzi huo akimshinda kwa mbali mpinzani wake, Raila Odinga.
Hii ni mara ya kwanza kwenye historia ya Afrika kwa Mahakama kufuta uchaguzi wa urais uliofanyika tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi ndani ya bara hilo.