Rais wa Zanzibar, Hussein Mwinyi Leo March 1, 2021 amemtangaza Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar kutoka Chama cha ACT- Wazalendo Othman Masoud Sharif kuwa mrithi wa marehemu Maalim Seif Sharif Hamad.

Taarifa iliyotumwa na kwa vyombo vya habari na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Zanzibar, Mhandisi Zena Said imesema Rais Mwinyi amezingatia kifungu cha 9(3) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Kifungu hicho kinasema, ‘Muundo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar utakuwa wa Umoja wa Kitaifa na utendaji wa kazi zake utafanywa katika utaratibu utakaohakikisha kuendelezwa kwa umoja nchini na kutimiza lengo la kufikia demokrasia.’

Hatua hiyo imekuja baada ya Chama cha ACT Wazalendo kukamilisha mchakato wa kupendekeza jina la atakayerithi nafasi hiyo katika kikao kilichoketi mwishoni mwa wiki iliyopita.

“Baada ya kushauriana na Chama cha ACT-Wazalendo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Hussein Mwinyi amemteua Othman Masoud Othman Sharif kuwa Makamu wa kwanza wa rais wa Zanzibar,” imesema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imesema uteuzi huo unaanza leo Machi Mosi na sherehe za kumuapisha Masoud zitafanyika kesho Machi 2 katika ukumbi wa Ikulu ya Zanzibar.

Majambazi watano wauawa, askari ajeruhiwa
Zitto: Tumempata mrithi wa Maalim Seif