Akisoma hukumu hiyo Jaji Mfawidhi Lameck M. Mlacha wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba na kumtia hatiani Mwalimu Respikius Patrick Mtazangira alisema Mahakama ilizingatia vigezo vingi hasa ushahidi uliowasilishwa Mahakani, jinsi mashahidi walivyowasilisha ushahidi wao lakini pia na washitakiwa wenyewe walivyojitetea ambapo mwisho imekuja kudhihirika wazi kuwa Mwalimu huyo alikuwa amekusudia kumuua mwanafunzi Spelius Eradius.
Katika hukumu yake Jaji Mfawidhi Mlacha alisema kuwa upande wa Mashitaka uliwakilishwa na Mawakili wanne walioongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali Hashim Ngole na upande wa utetezi uliwakilishwa na Mawakili wanne waliongozwa na Projestus Mulokozi lakini pia upande wa utetezi uliwakilishwa na Mawakili wengine wawili wa ziada Wakili Aron Kabunga na Aneth Rwiza.
Jaji Mfawidhi Mlacha alisema kuwa pamoja na Mawakili wa pande zote mbili kubishana kisheria kwa baadhi ya mambo lakini kuna mambo muhimu hayakubishaniwa nayo ni kwamba Washitakiwa wote wawili walimfahamu mwanafunzi Spelius Eradius, Walikiri kuwa Spelius Eradius alituhumiwa kuiba pochi na kupigwa, Mwili wa Spelius Eradius ulikutwa na majeraha, Mwalimu Erieth Gerald alipokelewa mizigo yake na wanafunzi na kutoa taarifa kwa mwalimu Mkuu kuwa amepotelewa na pochi yake.
Pia Mwalimu Erieth alitoa taarifa kwa mwalimu Respikius Patrick Mtazangira kuwa pochi yake imepotea pia washitakiwa wote wawili walikutwa na mwanafunzi Spelius Erdius kabla ya kukutwa na mauti ya kifo. Jaji Mfawidhi Mlacha alisema kuwa maelezo ya washitakiwa wote wawili yalitia shaka kuhusu kipigo cha Spelius Eradius.
Akimtia hatiani Mwalimu Respikius Patrick Mtazangira Jaji Mlacha alisema pia aliangalia sheria ya Elimu ya mwaka 2002 kifungu cha 60 na kanuni zake kuhusu adhabu ya viboko kwa mwanafunzi. Kanuni ya kwanza inasema kuwa adhabu ya kiboko itolewe kwa mwanafunzi kama amekosa kosa kubwa, pili anayeruhusiwa kumpiga mwanafunzi ni Mwalimu Mkuu au msaidizi wake au mwalimu aliyechaguliwa kupiga.
Tatu lazima adhabu ya kiboko izingatie afya ya mtoto umri na na visizidi viboko vinne tu, Nne adhabu hiyo iandikwe kwenye kitabu maalum jina la mtoto na idadi ya viboko alivyopigwa, tano mtoto achapwe mikono au matakoni na fimbo nyepesi inayonyumbuka na hairuhusiwi kuchapwa sehemu nyingine yoyote, sita mtoto wa kike achapwe na mwalimu wa kike au mwalimu Mkuu au mwalimu aliyeruhusiwa, saba Mtoto atakayekataa kuchapwa afukuzwe shule, nane Mwalimu atakayekiuka kanuni hizo achukuliwe hatua.
Mwalimu Respikius Patrick Mtazangira alitiwa hatihani kwasababu hakuwa na ruhusa ya kumpiga au kumchapa mwanafunzi Supelius Eradius pia alizuiwa na Mwalimu Mkuu Msaidizi hakusikia, alimchapa mwanafunzi huyo na fimbo isiyoruhusiwa (Vipande vya kuni) na mwisho hakuandika adhabu hiyo kwenye kitabu maalum.
Mwalimu Erieth Gerald Mahakama ilimwachaia huru kwa kuwa ushahidi uliotolewa dhidi yake wa kumchapa Mwanafunzi Supelius Eradius uliikanganya Mahakama na kuamua kuwa pengine si wa kweli ambapo pia Jaji Mlacha alisema kuwa kilichoangaliwa si pochi iliyokuwa imepotea bali ni kipigo kilichosababisha kifo cha mwanafunzi huyo na upande wa mashitaka ulishindwa kuthibitisha mashitaka dhidi ya mwalimu huyo.
Mara baada ya hukumu hiyo kutoka Wakili Mkuu wa Serikali aliyeongoza jopo la Mawakili upande wa mashitaka alisema kuwa upande wao wamerdhika na maamuzi ya Mahakama na wanaishukuru Mahakama hiyo kwa kutenda haki.