Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli leo ametengua uteuzi wa viongozi watatu wa Mkoa wa Arusha ikiwa ni pamoja na Mkuu wa Mkoa huo, Mrisho Gambo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, Juni 19, 2020 na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Rais Magufuli amemteua Idd Kimanta kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Kabla ya uteuzi huo, Kimanta alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Monduli ya mkoa huo.
Aidha, Rais Magufuli pia ametengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqaro na kumteua Kenan Kihongosi aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo.
Mkuu huyo wa nchi pia ametengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dkt. Maulid Madeni na amemteua Dkt. John Pima kushika nafasi hiyo. Kabla ya kuteuliwa leo kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Dkt. Pima alikuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora. Kuziba nafasi yake, Rais amemteua Jerry Mwaga kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kaliua.
Wateule hao wapya watafika Ikulu jijini Dar es Salaam, Jumatatu, Juni 22, 2020 kwa ajili ya hatua zaidi, kwa mujibu wa taarifa ya uteuzi huo.