Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa wagonjwa wengine wawili wa Corona wamebainika nchini. Hivyo, kufanya idadi ya wagonjwa kufikia watatu.
Akizungumza leo, Machi 18, 2020, Waziri Mkuu amesema kuwa mgonjwa mmoja amepatikana visiwani Zanzibar ambaye ni raia wa Ujerumani na mwingine ni raia wa Marekani aliyepatikana jijini Dar es Salaam. Mgonjwa wa kwanza aliyetangazwa juzi, ni Mtanzania aliyeingia nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) akitokea nchini Ubelgiji.
Aidha, Waziri Mkuu ametangaza kufunga vyuo vyote nchini ikiwa ni siku moja baada ya kutangaza kufunga shule zote za awali, msingi na sekondari. Pia, aliagiza mikusanyiko yote ya matukio ya kimichezo na burudani kusitishwa kama hatua za kuchukua tahadhari dhidi ya virusi hivyo.
Waziri Mkuu pia alitangaza kusitishwa kwa mikutano, warsha, semina na makongamano ya taasisi zote za Serikali na binafsi na kutoa elimu ya kuhusu jinsi ya kujikijnga. Alisema Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutenga maeneo ya karantini.
“Serikali imetenga Hospitali maalum za Mloganzila (Dar es Salaam), Kituo cha Busweru (Mwanza), Hospitali ya Mawenzi (Kilimanjaro), Mnazi Mmoja (Zanzibar), Chakechake (Pemba) kwa ajili ya kutoa huduma kwa waathirika,” amesema Waziri Mkuu.
Aliongeza kuwa sambamba na hatua hiyo, Serikali inatoa mafunzo kwa watumishi wa wizara ya afya ili kuwajengea uwezo wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.
Serikali imetoa Sh 500 milioni zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya Mbio za Mwenge wa Uhuru ili zitumike katika kuwezesha mapambano dhidi ya virusi vya corona, kama alivyoagiza Rais John Magufuli.