Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye ametangaza rasmi kukihama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuhamia katika umoja unaoundwa na vyama vikubwa vya upinzani, Ukawa.

Sumaye ametangaza uamuzi wake mbele ya waandishi wa habari muda mfupi uliopita, Kunduchi, Dar es Salaam akiwa na viongozi wa vyama vinavyounda Ukawa pamoja na mgombea urais wa umoja huo, Edward Lowassa.

Waziri Mkuu huyo ameeleza kuwa anahamia katika umoja huo ili kuongeza nguvu ya kuiondoa madarakani CCM kama inavyoonekana kuwa watanzania wengi wanahitaji mabadiliko.

“Sitoki CCM labda kwa sababu nina hasira na CCM, sitoki CCM kwa sababu labada nilishindwa katika kugombea urasi, sitoki CCM kwa sababu labda simpeni Magufuli. Bali natoka CCM kwa sababu nataka kuiimarisha CCM,” Alisema Sumaye na kudai kuwa anataka kuiimarisha CCM.

Alieleza kuwa anataka kuongeza nguvu kwenye kambi ya upinzani ili CCM ipate upinzani mzito zaidi na iimarike. Lakini anaamini kuwa mwaka huu kuna kila dalili kuwa upinzani utashika dola hivyo anataka kuongeza uzoefu katika serikali mpya.

Ameongeza kuwa wakati akiwa CCM alionekana kama hana umuhimu lakini kwa kuwa yuko upinzani na ameingia kuongeza nguvu anaamini wapinzani watauona umuhimu wake na pia CCM watauona umuhimu wake wakati huu.

Ingawa hakutaja chama alichojiunga nacho katika umoja huo, Sumaye alisema kuwa alifanya maamuzi hayo bila shinikizo la aina yoyote wala kupewa chochote na uongozi wa Ukawa bali amefanya kwa kuwa anataka upinzani uimarike zaidi na uongoze serikali ya awamu ya Tano.

“Hakuna chama tawala duniani kinachotawala nchi miaka yote, hakuna,” alisema.

Frederick Sumaye alikuwa waziri Mkuu wa serikali ya awamu ya tatu hivyo amejiunga na aliyekuwa waziri mkuu wa awamu ya nne.

 

 

 

Kilichomkera Zaidi Sumaye CCM, Alijeruhiwa Muda Mrefu
Kuhusu Mgombea Ubunge Wa Chadema Aliyevamiwa...