Rais wa Afghanistan, Ashraf Ghani ameikimbia nchi hiyo leo, muda mfupi baada ya wapiganaji wa Taliban kulizingira jiji la Kabul, ambalo ndilo makao makuu ya nchi hiyo.
Abdullah Abdullah, Mkuu wa Baraza la Usuluhishi la Taifa, ameiambia The Associated Press, akithibitisha kuwa Rais Ghani ameikimbia nchi, huku akilaani kitendo hicho.
“Rais ameikimbia Afghanistan, ameiacha nchi kwenye wakati mgumu sana. Mwenyezi Mungu atamuwajibisha,” amesema Abdullah.
Kundi la Taliban lilitangaza mapema leo kuwa litaingia ndani ya jiji la Kabul, hatua ambayo ilizua taharuki zaidi huku helikopta zikionekana kutua juu ya paa la Ubalozi wa Marekani kwa lengo la kuwachukua wanadiplomasia na watu wengine wanaoondoka nchini humo.
Imeelezwa kuwa kulikuwa na moshi mzito juu ya paa la ubalozi wa Marekani kutokana na zoezi la kuchoma moto nyaraka muhimu.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la AP, nchi nyingine za Magharibi pia zimeweka mpango wa haraka wa kuwaondoa watu wao waliokuwa wanafanya kazi maalum nchini Afghanistan.
Mamia ya watu walipanga foleni kwenye mashine za kutolea pesa kwa lengo la kuchukua hazina zao, huku wengine wakikimbia na kuacha mali zao wakielekea nchi za jirani.
Hatua ya Taliban kulishika jiji la Kabul ndani ya wiki moja imekuwa ya kushtua, kwani Jeshi la Marekani lilitoa tathmini kuwa huenda ikachukua mwezi mmoja hadi kundi la wapiganaji kulifikia jiji la Kabul.
Taliban wamepata nafasi ya kuteka majiji 24 muhimu zaidi ya nchi hiyo kati ya majiji 34, ikiwa ni siku chache tangu Marekani ilipotangaza kuwa inawaondoa wanajeshi wake wote nchini Afghanistan.
Rais wa Marekani Joseph Biden amesisitiza kuwa hatawarejesha wanajeshi wake nchini Afghanistan baada ya kukamilisha operasheni iliyodumu kwa miaka 20. Amesema kama Serikali ya Afghanistan haiwezi kuilinda nchi yake kwa kutumia vyombo vyake vya usalama, Marekani haiwezi kutumia rasilimali zake kuingilia vita ya wenyewe kwa wenyewe katika nchi ya ugenini.
Taliban wanaingia tena madarakani baada ya kuondolewa na Marekani miaka 20 iliyopita. Taliban ikiwa chini ya utawala wa Mullah Omar Mullah, ilimpa hifadhi Osama Bin Laden, Kiongozi wa Al-Qaeda na ikakataa kuwapa Marekani baada ya shambulizi la Septemba 11, 2001.
Marekani ilivamia Afghanistan kwa lengo la kumsaka Osama Bin Laden na wapiganaji wa Al-Qaeda. Ikakabiliana vikali na Taliban, na baadaye wapiganaji hao waliamua kuiachia Serikali na kukimbilia milimani. Marekani ilisaidia upatikanaji wa Serikali iliyochaguliwa kidemokrasia ambayo iliiunga mkono. Kwa miaka yote 20 Taliban wamekuwa mwiba wa ubavuni kwa Serikali hiyo.
Rais Biden amesema kwakuwa wameshamkamata na kumuua Osama Bin Laden miaka kumi iliyopita, wamedhoofisha kundi la Al-Qaeda katika eneo hilo, sasa ni wakati wa kurejesha wanajeshi wake nyumbani.
Rais Biden amesema Marekani imetumia zaidi ya $1 trilioni katika kuweka ulinzi na kuwapa mafunzo wanajeshi na polisi wa Afghanistan kwa kipindi hicho na haitaendelea kutumia rasilimali zake katika hatua hiyo.