Rais Dkt. John Pombe Magufuli amefuta agizo lililotolewa jana na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe linalotoa sharti kwa watu wote watakaofunga ndoa kuanzia tarehe 01 Mei, 2017 kuwa na cheti cha kuzaliwa.
Rais Magufuli amefuta agizo hilo leo Machi 17, 2017 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma muda mfupi kabla ya kuondoka na kurejea Jijini Dar es Salaam.
Rais Magufuli amesema mpaka sasa idadi ya Watanzania walio na vyeti vya kuzaliwa ni chini ya asilimia 20 huku wengi wao wakiwa ni wananchi waishio vijijini ambako ni vigumu kupata vyeti hivyo, na wengine wakiwa ni waliozaliwa kabla ya kuanza kutolewa kwa vyeti vya kuzaliwa nchini mwaka 1961.
Hivyo Rais Magufuli amesema Serikali haiwezi kuruhusu sharti hilo kutumika kwa kuwa litawanyima haki ya kuoa na kuolewa Watanzania wengi ambao hawana vyeti vya kuzaliwa, huku utaratibu wa kupata vyeti hivyo ukiwa bado unakabiliwa na changamoto nyingi kwa wanaohitaji.
Baada ya kufuta agizo hilo Rais Magufuli amewataka Watanzania wasiwe na wasiwasi wowote, na waendelee na utaratibu wa kuoa na kuolewa kama kawaida.
“Kama kuna kifungu chochote cha sheria kinachomlazimisha mtu awe na cheti cha kuzaliwa ndipo aoe ama aolewe nitamuelekeza Waziri wa Katiba na Sheria Harrison Mwakyembe apeleke Bungeni kikarekebishwe”- amesema Rais Magufuli.
Aidha, Wanasheria wametakiwa kuziangalia vizuri sheria zinazohusiana na kuzaliwa na kifo na kuoa na kuolewa ili zisilete mkanganyiko kwa wananchi, huku Watanzania wakitakiwa kuendelea kupata vyeti vyao vya kuzaliwa kama kawaida na amewataka viongozi wote kuwahamasisha wananchi kuwa na vyeti hivyo.