Kiungo kutoka nchini Ureno Bruno Fernandes huenda akakosekana katika mchezo wa leo Alhamisi (April 27) dhidi ya Tottenham baada ya kupata majeraha walipocheza dhidi ya Brighton katika Nusu Fainali ya Kombe la FA mwishoni mwa juma lililopita.
Manchester United itakuwa ugenini jijini London kucheza dhidi ya Tottenham katika mwendelezo wa Michezo ya Ligi Kuu ya England ‘Premier League’.
Bruno anatajwa kuwa huenda akawa sio sehemu ya mchezo huo kwani alilazimika kutoka kwenye mchezo wa Kombe la FA baada ya kuumia Kifunzo cha Mguu ‘ENKA’.
Katika mchezo huo, kiungo huyo aliumia mapema na matumaini ya Man United kuona anapona haraka na kucheza dhidi ya Tottenham japo sio kwa asilimia 100.
Man United baada ya leo kucheza na Tottenham, mchezo ujao utakuwa dhidi ya Aston Villa.
Jumatatu ya juma hili, Bruno alionekana amevaa kiatu maalum cha kumlinda miguu akiwa anataembelea gongo na hii ikiashiria huenda asiwe fiti kwa mchezo wa leo.
Ripoti za ndani zinaeleza kwamba, Bruno atakosa mchezo wa Tottenham na Aston Villa.
Kiungo huyo amekuwa nyota muhimu wa kikosi cha Kocha Erik ten Hag.
Bruno amefunga mabao 10 na asisti 13 katika mechi 50 msimu huu, amekuwa nahodha hasa anapokosekana Harry Maguire.
Kama atakosekana basi litakuwa ni pigo kubwa kwa Ten Hag kwani viungo wake wengine wapo nje kama Donny van der Beek, Scott McTominay, huku wachezaji wengine kama Alejandro Garnacho, Lisandro Martinez na Raphael Varane nao ni majeruhi.
United kwa sasa imesalia na mechi tisa zikiwemo nane za Premier na fainali ya FA dhidi ya Manchester City.