Beki kutoka nchini Uholanzi na klabu ya Stoke City Bruno Martins Indi atakosa mchezo wa ligi wa mwishoni mwa juma hili dhidi ya Crystal Palace, kufuatia maumivu ya nyonga yanayomkabili.
Meneja wa Stoke City Paul Lambert amezungumza katika mkutano na waandishi wa habari hii leo na kueleza maendeleo ya beki huyo ambaye alikua sehemu ya kikosi cha Uholanzi kilichoshiriki fainali za kombe la dunia mwaka 2014.
Martins Indi alicheza dakika 52 mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Liverpool, lakini alishindwa kuendelea na mchezo huo uliomalizika kwa matokeo ya sare ya bila kufungana, baada ya kuumia sehemu za nyonga ya mguu wake wa kushoto.
“Tutamkosa Martins Indi katika mchezo wetu na Crystal Palace mwishoni mwa juma, lakini tumejiandaa kupambana, na pengo lake litazibwa kikamilifu,” Amesema Lambert.
“Imekua bahati mbaya kwetu kumkosa mchezaji muhimu kama huyu, lakini tunatarajia huenda akarejea kikosini mwishoni mwa juma lijalo tutakapocheza dhidi ya Swansea City, kwa sababu anaendelea kupatiwa matibabu, na hali yake inaridhisha.”
Stoke City inashika nafasi ya pili kutoka chini kwenye msimamo wa ligi ya nchini England, ikiwa na alama 30, lakini bado ina nafasi kubwa ya kujinasua kwenye mtego wa kushuka daraja kutokana na tofauti ya alama mbili iliopo dhidi ya Southampton wanaoshika nafasi ya 17,huku Swansea city wanaokamata nafasi ya 16 wakiwazidi alama tatu.