Nahodha na mlinda mlango wa klabu bingwa nchini Italia Juventus, Gianluigi Gigi Buffon, anaamini mpambano wa hii leo utakaowakutanisha na Man City kwenye uwanja wa ugenini, unapaswa kuwa kipimo kizuri kwao kama sehemu ya mafanikio waliyoyakusudia kwa msimu huu.

Buffon, amesema mchezo huo unapaswa kutumiwa kama kipimo kwao, kutokana na kikosi chao kuanza vibaya katika kampeni ya kusaka ubingwa wa nchini Italia hali ambayo imeshaanza kuleta tafrani baina ya mashabiki wao.

Mlinda mlango huyo amesema pamoja na ligi kuwa na michezo mingi bado kuna haja kwa wadadisi wa soka kuutazama mchezo wa hii leo wa michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, kwa ajili ya kupima kama watakua wanatosha kufikia lengo walilojiwekea tangu mwanzoni mwa msimu huu.

Amesema mchezo wa leo una changamoto kubwa sana kwa kikosi cha Juventus kutokana na umahiri wa timu ya Man City ambao utawapa changamoto tofauti na timu za nchini Italia.

Buffon mwenye umri wa miaka 37 ameongeza kuwa timu za nchini Italia wakati mwingine zimekua zikicheza dhidi ya Juventus kwa kukamia zaidi, na wakati mwingine zimekua zikifanikiwa kupata matokeo mazuri, hali ambayo kwake hadhani kama ni kipimo kizuri cha kuipima klabu yao ambayo imekua ikifanya vyema kwa misimu minne iliyopita.

Mpaka sasa Juventus imeshacheza michezo mitatu ya ligi ya nchini Italia na imeambulia point moja baada ya kupata matokeo ya sare ya bao moja kwa moja dhidi ya ChievoVerona mwishoni mwa juma lililopita, lakini mambo yalikua tofauti kwenye michezo iliyotangulia baada ya kufungwa mabao mawili kwa moja dhidi ya AS Roma na kabla ya hapo Udinese waliwakandamiza wambingwa hao kwa kuwafunga bao moja kwa sifuri katika mchezo wa ufunguzi.

Yanga Yapewa Masharti Ya Kufanya Uchaguzi
TFF Na Kampeni Za Vyama Vya Siasa