Neema ya wanabunda kumpokea Esther Bulaya aliyehamia Chadema akitokea CCM kuwa mgombea ubunge wa jimbo la Bunda Mjini imegeuka changamoto kwa Chama chake hicho kipya.

Uamuzi wa Kamati Kuu ya Chadema Taifa kumteua Esther Bulaya kugombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya chama hicho huku ikimuacha mwanachama aliyeshinda katika kura za maoni, Pius Masururi kumepelekea mgawanyiko baada ya mwanachama huyo kuhamia CCM akipinga uamuzi huo.

Akiongea jana na Mazingira Fm ya mjini humo muda mfupi baada ya kutangaza uamuzi wa kujiunga na CCM, Masururi alisema kuwa Kamati Kuu ya Chadema haikumtendea  haki kwa kumuengua katika nafasi hiyo bila kuzingatia mchango wake katika kukijenga chama hicho kwa zaidi ya miaka minne.

Masururi ameungwa mkono na viongozi wengine wa ngazi za juu waliotangaza kujiuzulu nyadhifa zao wakieleza kuwa kilichofanywa na Kamati Kuu ya Chama hicho ni ukiukwaji wa katiba ya chama .

Waliotangaza uamuzi huo ni pamoja na Alfred Imanani (Mwenyekiti wa  Jimbo), Emmanuel Malibwa (Katibu Mwenezi), Dickson Kujerwa (Mwenyekiti BAVICHA), Mwenge Webiro (Katibu BAWACHA jimbo),Ng’wena Mwita (Mwenyekiti Baraza la Wazee  Jimbo), Kibago Kibago (Red Brigedia Mkuu).

“Mimi pamoja na viongozi wa jimbo na Kamati ya UTENDAJI Jimbo la Bunda tumejiuzulu baada ya kutoridhika na uamuzi wa Kamati Kuu lakini pia baadhi ya makatibu na wenyeviti katika kata 20 za jimbo hili wamejiuzulu na watabaki kuwa wanachama wa kawaida wa Chadema,” alisema Katibu wa Chadema Wilaya ya Bunda, Rita Ikandire.

Hata hivyo, mmoja wa viongozi wa ngazi za juu wa Wilaya ya Bunda, Kaunya Yohana  alipinga maelezo yaliyotolewa na viongozi hao akidai kuwa hawakujiuzulu bali walisimamishwa uongozi kwa barua.

“Viongozi hawa hawajajiuzulu kama wavyodai, ukweli ni kwamba wamesimamishwa uongozi tangu Agosti 15 mwaka huu mpaka mambo yakatapokuwa sawa. Wamesimamishwa kupitia barua yenye kumbukumbu Na. C/HQ/ADM/KK/08 ya tarehe Agosti 19, 2015,” alisema Yohana.

Diamond Akamilisha Collabo Na Ne-Yo, Aitabiria Mema
UVCCM Yatoa Onyo Chadema Kutumia Red Brigade