Wakina mama katika Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera wameishukuru serikali kwa namna inavyoendelea kuwaboreshea huduma za Afya kwa kuwajengea kituo bora cha afya cha Zamuzamu kitakachoweza kuwahudumia wananchi zaidi ya elfu kumi pindi kitapokamilika.
Wametoa shukrani zao mbele ya kamati ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya Bukoba mjini ilipofika katika kituo hicho kufanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika manispaa hiyo, ambapo wamesema kuwa wamekuwa wakipata shida wakati wa kujifungua na kusababisha mrundikano katika hospitali ya rufaa.
Wamesema kuwa msaada wa vifaa tiba vilivyotolewa na mbunge wa viti maalumu wa CCM Mkoa Kagera, Halima Bulembo utasaidia sana kinamama waliokuwa wakitaabika kutokana na uhaba uliokuwepo kituoni hapo.
Kamati hiyo iliyoongonzwa na mwenyekiti wa CCM manispaa ya Bukoba, Muganyizi Zachwa iliambatana na mbunge wa viti maalumu CCM Mkoa Kagera anayewakilisha vijana, Halima Bulembo ambaye ameunga mkono jitihada za serikali kwa kutoa msaada wa vifaa tiba ambavyo ni Vitanda, Magodoro, Mashuka na vifaa vingine vya kutumia wanawake wakati wa kujifungua katika kituo hicho.
“Mimi kama mama na mbunge wa vijana Mkoa wa Kagera naunga mkono juhudu hizi za serikali ya awamu ya tano, hiki nilichojaaliwa naomba mkipokee Wanabukoba na nitoe wito kwa wadau wengine kuendelea kusaidia vitu vingine katika mkoa wetu,”amesema Bulembo
Kwa upande wake Mganga mkuu wa Manispaa ya Bukoba, Dkt. Hamza Mugula ameshukuru kupatiwa msaada huo na kusema kuwa vifaa hivyo vitaanza kutumika katika majengo mapya yanayoelekea kukamilika ambapo pia ujenzi wake umefikia aslimia 98.
Kamati ya siasa imeendelea na ziara yake katika shule ya sekondari Bukoba iliyoharibiwa na upepo mkali ulioambatana na mvua kali ambayo ujenzi wake unaaendelea chini ya kampuni ya Mzinga Investiment kutoka mkoani Morogoro, ambapo wameridhishwa na ujenzi huo ambapo wamemuomba mkandarasi kuongeza kasi ili wananfunzi waanze kuitumia shule ile.