Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo amepinga zoezi la bomoabomoa linaloendelea katika baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam akidai kuwa zoezi hilo linamjengea chuki rais John Magufuli kwa wananchi waliomuamini kuwa atawaletea neema.

Akizungumza katika mahojiano maalum na gazeti la Mwananchi, Bulembo alilitaka NEMC kusitisha zoezi hilo katika maeneo yaliyo nje ya bonde la Jangwani na Bonde la Msimbazi ambayo yako katika maeneo hatarishi.

Alisema kuwa kuendeleza zoezi hilo la kuvunja nyumba za wananchi ni kuvunja imani ya wananchi kwa rais Magufuli.

“NEMC wasiwe kama wameshuka kutoka mbinguni na kukuta watu wamejenga mabondeni. Wasituharibie imani ya wananchi kwa Rais,” alisema Bulembo.

“Kwani (NEMC) walikuwa wapi siku zote mpaka wafanye shughuli hiyo kwa sasa baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani? Sikubaliani na bomoabomoa hiyo isipokuwa hiyo ya Jangwani na sehemu hatarishi na Bonde la Msimbazi,” aliongeza.

Alieleza kuwa watu ambao walikuwa wamekaa katika maeneo yaliyokaribu na mabondeni kwa miaka zaidi ya 30 na hawajawahi kukumbwa na maafa hawapaswi kubomolewa nyumba zao kama inavyofanywa hivi sasa.

“NEMC waache kuleta hasira za wananchi kwa Rais wao, walikuwa wapi mpaka wanasubiri sasa?” Bulembo alihoji.

Bulembo alikuwa msitari wa mbele kwenye kampeni za urais akizunguka na rais John Magufuli kwa siku zote 52 za kampeni. Hivi karibuni, Bulembo alimtembelea rais Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam.

Baba Azaa na binti yake watoto wanane
Audio: Wastara Alia na Ushiriki wake kwenye Kampeni na Kinachotokea kwenye Bomoabomoa