Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Young Africans Hassan Bumbuli amemlipua Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally, kufuatia kauli aliyoitoa jana Jumatano (Februari 02), akiwa kwenye mahojiano kwenye kituo cha Televisheni cha ETV.

Ahmed Ally aliibutua Young Africans kwa kusema klabu hiyo imezoea kukaa kileleni na kuzurura hapo, kisha inaporomoka, huku akiamini kikubwa msimu huu klabu hiyo ya Jwangani imeongeza ‘MAKELELE’ na sio Ubora wa kikosi.

Bumbuli amesema maneno hayo ya Ahmed Ally ni mtazamo wake binafsi na anamtazama kama bwana mdogo katika tasnia ya kuusemea mpira wa Tanzania katika upande wa vilabu.

“Ni mtazamo wake binafsi, siwezi kumuingilia na kusema lolote kuhusu hilo alilolisema, halafu huyu jamaa bado mdogo na mchanga sana katika tasnia hii ya ya usemaji, kwa hiyo naheshimu huo mtazamo wake na aendelee hivyo hivyo kama anadhani hiyo ndio njia sahihi ya kuisema klabu yake.”

“Mimi Hassan Bumbuli nimejiwekea misingi ya kutozungumza chochote kuhusu upande wa pili kila ninapopata nafasi ya kuhojiwa katika vyombo vya habari, na nikizungumzia labla kama kuna jambo na mno mno sana, huwezi kuniuliza kwenye mahojiano nikakujibu kuhusiana na upande wa pili.”

“Wao wana mambo yao, wana mipango yao wadili na wazee wao, sisi tuna mambo yetu na mipango yetu na tunadili na mambo yetu, haya mambo ya kwenda kwenye mahojiano kila siku unawazungumzia wenzio unaonekana wewe huna ajenda.” amesema Bumbuli.

Kuhusu mipango ya Ubingwa wa Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’, Bumbuli amesema Young Africans imejizatiti kisawa sawa licha ya kuwepo kwa maneno ya kejeli kutoka kwa watani zao wa jadi, wakidai wanaongoza Ligi Kuu kwa muda kisha watashuka na kuwapisha wao ili watete ubingwa.

“Waendelee kuamini hivyo, ni imani yao ambayo wamekua nayo kwa hiyo tunawatakia kila la heri katika kuamini hivyo, ili mwisho wa msimu tutakuja kuzungumza na wanahabari popote pale tutakapojaaliwa In Shaa Allah.

Young Africans inaongoza Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa alama 35, wakiiacha Simba SC inayoshika nafasi ya pili kwa tofauti ya alama 10, huku kila mmoja akicheza michezo 13 hadi sasa.

Mlinda Lango Tanzania Prisons akataa kuingia mtegoni
Jemedari Said awachana waamuzi Ligi Kuu