Uongozi wa klabu ya Young Africans umetoa sababu za kumsajili kiungo mzawa Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ aliyeihama Azam FC na kutua kwa Wananchi katika kipindi hiki cha Dirisha Dogo la Usajili.
Usajili wa kiungo huyo aliyeigomea Azam FC baada ya kutakiwa kurejea kambini kufuatia adhabu aliyopewa mwanzoni mwa msimu huu, ulikamilishwa kati kati ya juma lililopita baada ya kuvunja mkataba wake na Wanalambalamba.
Uongozi wa Young Africans umesema umemsajili ‘Sure Boy’ kutokana na uwezo wake uwanjani na si mapenzi yake kwa klabu hiyo kama wengine wanavyodhani.
Akizungumzia usajili wa mchezaji huyo, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Young Africans Hassan Bumbuli amesema ‘Sure Boy’ hakuwa kwenye malengo kwa kipindi hiki cha usajili kama wengi wanavyodhani, lakini baada ya kuachana na klabu yake na kumruhusu kuondoka ndipo na wao wakaanza utaratibu kama wanaweza kumsajili, na bahati nzuri wakafanikiwa.
“Young Africans haisajili mchezaji kwa mapenzi, ila uwezo wake sisi tulihitaji kiungo mchezeshaji ili kama Khalid Aucho hayupo, basi huyu anacheza. Kocha anahitaji kuwa na machaguo mengi, akitoa moto anaingiza moto, siyo akitoa moto anaingiza maji ya vuguvugu,” amesema Bumbuli.
Akisimulia jinsi kiungo huyo alivyosajiliwa, amesema ilikuwa ni kama bahati kwani tayari walikuwa wanafanya mazungumzo na mchezaji mmoja nje ya nchi.
“Tulikuwa tunafanya mazungumzo na mchezaji mmoja nje ya nchi kiungo mchezeshaji, mara tunasikia jamaa ameachana na timu yake, usiku huo huo tukapigiana simu viongozi tukaambizana kama kuna uwezekano wa kuonana na meneja wake, Heri Mzozo, yaani mpaka asubuhi tu inafika kila kitu tayari, ilikuwa kama kuokota dodo chini ya mwarobaini,” amesema.
‘Sure Boy’ ameihama Azam FC baada ya kuitumikia kwa miaka 14 kutoka mwaka 2007-2021 akiwa sehemu ya wachezaji wakongwe waliokua wamesalia Azam Complex Chamazi.