Uongozi wa Young Africans umekanusha taarifa za kupokea ofa kutoka Horoya AC inayomlenga kiungo kutoka DR Congo Mukoko Tonombe, ili ajiunge na klabu hiyo ya nchini Guinea mwishoni mwa msimu huu.

Uongozi wa klabu hiyo kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, umekanusha taarifa hizo kufuatia kuzuka tetesi nyingi kwenye mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari zinazodai kuwa kiungo huyo anawaniwa na Hoyoya AC.

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Young Africans, Hassan Bumbuli amesema hawajui chochote kuhusu suala hilo na wenyewe wanaona kwenye mitandao ya kijamii.

Bumbuli amesema kama Horoya AC wanamtaka Mukoko watawafuta na kukaa nao chini kuzungumza nao lakini kwa sasa wameelekeza nguvu kwenye mchezo wa leo wa Robo Fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi ya Mwadui FC.

“Hata sisi tunaona kwenye mitandao ya kijamii kuhusu Mukoko lakini hakuna ofa yoyote, macho yetu ni kesho dhidi ya Mwadui,” amesema Bumbuli.

Tetesi kuhusu Mukoko kuwaniwa na Horoya AC, zimedai kuwa tayari uongozi wa klabu hiyo ya Guinea imejipanga kutuma ofay a Dola za Kimarekani laki mbili (200,000), huku ikijipanga kumlipa mshahara Mukoko wa Dola za kimarekani 9,000 (Sh18 milioni) kwa mwezi.

RC Makalla awaonya majambazi Dar
Ajira za walimu gumzo Bungeni