Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Young Africans Hassan Bumbuli ametoa sababu za kuialika Mafunzo FC kutoka Zanzibar, kwa ajili ya mchezo wa Kirafiki utakaopigwa leo Jumatano (Machi 30), Uwanja wa Azam complex Chamazi.

Young Africans itacheza mchezo huo wa Kirafiki kujiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaowakutanisha na Azam FC April 06, Uwanja wa Azam complex Chamazi.

Bumbuli amesema wameamua kuialika Mafunzo FC kwa sababu hawajawahi kucheza nayo, hivyo watapata kitu kipya, tofauti na timu zingine za Bara na Visiwani ambazo nyingi tayari wameshakutana nazo.

“Tumecheza na timu nyingi za Zanzibar, lakini hatujawahi kucheza na Mafunzo kwa muda mrefu, tumeona tucheze nayo kwa sababu huenda inaweza kutupa kitu kipya ambacho hatujawahi kukutana nacho na tukajifunza, na hizi za Tanzania Bara, karibuni zote tumecheza nazo kwenye mzunguko wa kwanza, kwa hiyo hatukuona kipya tutakachokwenda kujifunza kutoka kwao,” amesema Bumbuli

Katika hatua nyingine Bumbuli amesema katika mchezo dhidi ya Mafunzo FC huenda mashabiki wakashuhudia urejeo wa kiungo Mshambuliaji kutoka DR Congo Jesus Moloko aliyekuwa majeruhi.

“Kocha wetu ametaka mchezo huu kwa ajili ya kuendelea kuwapa wachezaji utimamu wa mwili, lakini pia tumesikia kilio cha wanachama na mashabiki wa Young Africans ambao wanasema hawataki kukaa muda mrefu bila kuiona timu yao ikicheza, kwa hiyo leo Jumatano (Machi 30) saa moja usiku tuko Chamazi, tukajumuike kule, tujazane ili tujue tarehe sita tukicheza na Azam Aprili 06 tujue tutakaaje.” amesema Bumbuli.

Urusi yapunguza wanajeshi wake Ukraine
Kocha Mafunzo FC aitahadharisha Young Africans