Mkutano wa Sita wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaanza leo mjini Dodoma.huku Serikali inatarajiwa kutoa kauli mbili kuhusu hali cha chakula nchini na deni la Taifa linaloenda sanjali na hali uchumi nchini.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Bunge, Owen Mwandumbya alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari.
Katika kikao hicho, kutakuwa na kiapo cha uaminifu kwa wabunge watatu wa Kuteuliwa na mmoja wa kuchaguliwa ambao ni Abdallah Bulembo, Profesa Palamagamba Kabudi na Anne Kilango Malecela (wote wa Kuteuliwa) na mbunge wa kuchaguliwa kutoka Jimbo la Dimani Zanzibar, Ali Juma Ali (Dimani-CCM).
Aidha, Kamati 14 za kisekta zitawasilisha taarifa mbalimbali ambazo zitajadiliwa na wabunge kadiri ratiba itakavyokuwa inaelekeza.
Hata hivyo, katika kikao hicho kunatarajiwa kuwasilishwa Miswaada mtatu ambayo ni Muswada wa Sheria ya Madaktari, Madaktari wa Meno na Watalaamu wa Afya Wasaidizi wa Mwaka 2006, Muswada wa Huduma za Msaada wa Kisheria wa Mwaka 2016 na Muswada wa Marekebisho Mbalimbali ya Sheria Namba 4 wa Mwaka 2016.