Kikao cha pili cha Bunge la kumi na moja linalotarajiwa kuwa na ushindani mkali wa hoja kati ya wabunge wa vya upinzani vinavyounda Ukawa na wabunge wa CCM kitaanza leo mjini Dodoma huku mambo saba muhimu yakitarajiwa kuibua mjadala mkubwa.

Suala la kwanza ni hujadili hotuba ya Rais John Magufuli aliyoitoa bungeni hapo mwaka jana katika kikao cha kwanza cha bunge hilo. Hapo suala la kupambana na ufisadi linatarajia kuleta hoja nzito zaidi kutoka kila upande. Hotuba ya Rais ilisifiwa na takribani kila mwananchi pamoja na wanasiasa mbalimbali.

Pili, Kurudiwa kwa uchaguzi Mkuu wa Zanzibar. Hili ni suala nyeti na linalopaswa kubebwa kwa uangalifu mkubwa. Wabunge wa Ukawa na CCM wanatarajiwa kurusha nanga zao za hoja na maoni katika kusaidia namna ya kupata muafaka. Bila shaka hapo mengi yataibuka na huenda kukawa na mgongano mkubwa wa hoja na mawazo.

Zoezi la Bomoabomoa pia linaweza kupewa nafasi yake katika Bunge hilo hususan katika utekelezaji wake na mapungufu yaliyojitokeza.

Maazimio ya Bunge juu ya sakata la ESCROW linaweza kuwa mada moto zaidi katika bunge hilo kwani tayari kumekuwa na vutankuvute kabla ya Bunge. Mbunge wa jimbo la Ubungo Saed Kubenea na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ambao ni mahasimu wa kisiasa wameonekana kuwa na nia moja katika kulirudisha bungeni sakata la ESCROW. Mmiliki wa Kampuni ya IPTL/PAP, Harbinder Singh Sethi amepinga mahakamani kurudishwa bungeni kwa sakata hilo lakini Zitto amesisitiza kuwa mtu binafsi hawezi kulizuia Bunge kutekeleza majukumu yake.

Utekelezaji wa sera ya elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne pia ni suala ambalo litaleta mjadala katika Bunge hilo, kwa kuzingatia changamoto zilizoanza kuripotiwa.

Uteuzi wa wajumbe wa kamati za Bunge ambao vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa vimeulalamikia na hata kutishia kuususia unatarajiwa kuwa sehemu ya hoja zitakazoleta mjadala mkubwa katika Bunge hilo.

Kadhalika, migogoro iliyoibuka katika chaguzi za Mameya wa majini na Manispaa pamoja na wenyeviti wa Halmashauri. Waziri wa TAMISEMI atakuwa na kazi ya kujibu hoja na maswali yatakayokuwa yanaelekezwa kwake kuhusu zoezi hilo.

Pamoja na hayo yote, hoja binafsi za wabunge zinatarajiwa kuibuliwa na kuleta mjadala mzito kwani tayari baadhi ya wabunge wamekwisha eleza nia yao ya kupeleka bungeni hoja binafsi kuhusu masuala mbalimbali.

Bunge hili linatarajiwa kuwa la kipekee  na lenye changamoto kubwa kwa kuwa na idadi kubwa ya vijana na idadi kubwa ya wabunge wa upinzani ambao wameunda umoja wao.

 

Rihanna awaandaa mashabiki kula ‘ANTI’ baada kukamilisha mapishi
Joseph Butiku aelekeza kinachotakiwa kufanyika Zanzibar