Katibu wa Bunge. Ndg. Nenelwa Mwihambi, ndc amesema vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania vitaanza kurushwa moja kwa moja kutoka Bungeni katika vipindi vyote vya bunge.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dodoma, Nenelwa amesema baada ya maboresho ya Studio ya Bunge na Kamati ya Uongozi ya Bunge kuridhia, vikao vya Bunge vitaanza kurushwa live kuanzia kesho tarehe 05 Aprili 2022 wakati Mkutano wa Saba wa Bunge mahsusi kwa ajili ya kupitisha Bajeti ya Serikali utakapoanza Bungeni Jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa Katibu wa Bunge, vituo vyote vya televisheni, radio na mitandao ya kijamii itaruhusiwa kujiunga na kurusha matangazo hayo ya vikao vya Bunge.
Bunge ni chombo cha kiserikali kilicho na jukumu la kutunga sheria, ambacho wawakilishi wake huchagliwa na wananchi.
Matangazo ya moja kwa moja ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yalizuiliwa na serikali mwaka 2016 kutokana na kile kilichotajwa kuwa ni matumizi makubwa ya pesa.