Bunge la Uingereza linatarajia kupiga kura kwa mara ya tatu hii leo, kupitisha sehemu ya makubaliano kwa taifa hilo kujiondoa kutoka katika Umoja wa Ulaya.
Kura ya leo itahusu tu makubaliano ya Uingereza kujiondoa, na sio tamko tofauti la kisiasa kuhusu mahusiano ya hali ya baadaye kati ya nchi hiyo na Umoja wa Ulaya.
Aidha, Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May anafanya kila jitihada za dakika za mwisho kuwashawishi wabunge kupitisha makubaliano hayo aliyofikia na Umoja wa Ulaya, lakini wataalam wanasema anakabiliwa na uwezekano wa kushindwa kwa mara nyingine.
Hapo awali siku ya leo ndio ilikuwa imepangwa Uingereza kujiondoa rasmi kwenye umoja huo, ambapo hatua ya Uingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya ilikumbwa na changamoto nyingi baada ya bunge kukataa mapendekezo mbadala manane ya Theresa May.
EU ilikuwa imekubali kusogeza mbele tarehe ya Brexit hadi Mei 22, iwapo makubaliano ya kujiondoa yataidhinishwa na bunge la Uingereza wiki hii, na endapo hawataidhinisha makubaliano hayo, mchakato wa kujiondoa utarefushwa hadi Aprili 12, ambapo Uingereza itahitajika kutoa mapendekezo jinsi ya kuendelea na mchakato wake wa kujiondoa kwenye Umoja huo.