Kwaya ya Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania, kwa mara ya kwanza leo imeimba katika ufunguzi wa mkutano wa 18 kikao cha kwanza cha Bunge la 11 kilichoanza Jijini Dodoma.
Spika wa Bunge, Jobu Ndugai ameipongeza kwaya hiyo ya bunge ambapo amesema leo imeimba vizuri wimbo wa Taifa na wajumuiya ya Afrika Mashariki wakati wa ufunguzi wa mkutano huo.
Awali, wimbo wa Taifa na wa Afrika Mashariki kwenye ufunguzi wa mikutano ya Bunge ulikuwa unaimbwa na kwaya ya Jeshi la kujenga Taifa (JKT) lakini leo umeimbwa na watumishi wa Bunge ambao walivaa majoho nadhifu ya mchanganyiko wa rangi nyeusi na blue.
Baada ya kumaliza kuimba na dua ya kuliombea Bunge na Taifa, Spika Ndugai alieleza kuwa hatua ya kwaya kuimba wimbo huo inatokana na uamuzi wa kamati ya uongozi ya Bunge uliotolewa Januari 2020.
Pia amelishukuru Jeshi la polisi Tanzania kwa kuwafundisha watumishi hao ambapo baada ya kuimba wabunge waliwapigia makofi na kuwapongeza.