Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania leo, Mjini Dodoma limepitisha muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali (Na. 4) wa mwaka 2016 [The written laws miscellaneous Amendments (No. 4) Bill, 2016].
Akiwasilishwa muswada huo Bungeni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju, amesema kuwa muswada huo unapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria Sita ambapo lengo la marekebisho yanayo pendekezwa ni kurahisisha utekelezaji wa Sheria hizo kwa kuondoa upungufu uliojitokeza wakati wa kutumia masharti ya sheria hizo.
Masaju amezitaja sheria zilizo pendekezwa kufanyiwa marekebisho kupitia muswada huo kuwa ni Sheria ya Mikopo, Misaada na Dhamana, Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, Sheria ya Kodi ya Mapato, Sheria ya Ardhi, Sheria ya Sukari na Sheria ya Hifadhi ya Wanyamapori.
“Ibara ya 21 ya muswada inapendekeza marekebisho katika kifungu cha 30 cha Sheria ambacho kina weka masharti kuhusu Waziri mwenye dhamana ya fedha kukasimu madaraka yake chini ya Sheria hiyo. Sheria ilivyo sasa inaelekeza kuwa Waziri anaweza kukasimu mamlaka yake ya kujadili mkopo (negotiating loan), kuingia makubaliano ya kukopa mkopo na kutoa dhamana,” amesema Masaju.
Aidha,amesema kuwa muswada unapendekeza kuwa Waziri awe na uwezo wa kukasimu pia mamlaka ya kujadili au kuingia makubaliano ya misaada kwa mamlaka au mtu mwingine. Lengo la marekebisho hayo ni kurahisisha taratibu za upokeaji misaada kwa kuwa sheria hiyo ilikuwa kimya kuhusu suala hilo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Katiba na Sheria, Mohamed Mchengerwa alipokuwa akitoa maoni na ushauri wa kamati hiyo alisema kuwa, kamati hiyo inaunga mkono marekebisho ya Sheria ya Mkopo wa Elimu ya Juu kwa sababu itatoa nafasi kwa Watanzania wengi wa kipato cha chini kupata nafasi ya kusoma katika Vyuo vya Elimu ya Juu.