Bunge la Marekani limefanikisha kura iliyoridhia Rais Donald Trump kushtakiwa kwenye Baraza la Seneti kwa matumizi mabaya ya madaraka, hali itakayoamua hatma ya urais wake.

Bunge hilo limepiga kura ambapo wabunge 230 ambao ni wengi wa chama cha Democratic wameshinda, huku wabunge wawili wa chama hicho wakipiga kura ya kupinga uamuzi huo.

Trump alipata utetezi wa kura zote za wabunge wa chama chake cha Republican lakini kwakuwa ni wachache, demokrasia ya ‘wengi wape’ ilichukua mkondo wake.

Hatua hiyo ilifikiwa kufuatia tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka akidaiwa kuishinikiza Serikali ya Ukraine kuwachukulia hatua Joe Biden na mwanaye ambao wanadaiwa kuwa watakuwa wapinzani wake kwenye uchaguzi ujao. Pia, anatuhumiwa kuingilia uchunguzi wa Bunge hilo dhidi yake.

Trump anakuwa Rais wa tatu wa nchi hiyo kufikia hatua ya kupigiwa kura ya matumizi mabaya ya madaraka katika historia. Hata hivyo, Bunge la Seneti linahitaji theluthi mbili ya kura ili kufanikisha kumuondoa madarakani, jambo ambalo sio rahisi kufanikisha kwa muundo wa Baraza hilo sasa.

Wakati hatua hiyo ikiendelea, Trump alikuwa akiwahutubia wafuasi wake na alikosoa vikali kinachofanywa na Bunge hilo.

“Wakati sisi tunaendelea kuongeza ajira na kuipigania Michigan, mlengo wa kushoto wa Bunge la Congress umejaa wivu, chuki na fujo, ninyi mnaona kinachoendelea,” alisema Trump.

Ikulu ya Marekani imetoa taarifa rasmi ikieleza kuwa Rais Trump amejaa imani na anajiamini kuwa Baraza la Seneti litakuwa upande wake.

Ibara ya Pili ya Katiba ya Marekani inaeleza kuwa, “Rais, Makamu wa Rais na Maafisa wote wa Marekani wanaweza kuondolewa ofisini kwa kupigiwa kura ya matumizi mabaya ya madaraka na kushtakiwa kwa uhaini, rushwa/hongo au makosa makubwa ya jinai.”

Zanzibar: Afariki kwa mchezo wa 'spot honda' Baharini
Kikongwe adai kuporwa ardhi yenye kaburi, vitindi vya ulanzi, aiangukia Serikali