Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imelishauri Bunge wakati wa utungaji Sheria ya Fedha ya Mwaka 2017 kuongeza tozo kwa kila lita ya mafuta ya dizeli na petroli.
Kamati hiyo imesema kuwa tozo hiyo iwe Sh. 100 badala ya Sh 50 kwa sababu Mfuko huo umeonyesha mafanikio makubwa katika kuwezesha upatikanaji fedha licha ya kiasi kinachopatikana kutokidhi mahitaji ya maji yaliyopo.
Aidha, akiwasilisha taarifa ya shughuli zilizotekelezwa na Kamati hiyo mwaka 2016 hadi 2017, Mwenyekiti wake Dkt. Christine Ishengoma amesema kuwa Kamati inashauri kuongeza tozo kutoka Sh 50 hadi Sh 100 kwa kila lita ya mafuta ya dizeli na petroli.
Vi vile amebainisha kuwa Kamati hiyo imebaini kuwa katika Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya mwaka 2016/17, katika fungu la fedha za maendeleo, Serikali ilitenga kiasi kikubwa cha fedha za ndani ikilinganishwa na fedha za nje, ambazo hazikutolewa.
“Hazitolewi kama zilivyoidhinishwa na Bunge, hivyo kuchangia kutofikiwa kwa malengo yaliyo pangwa, hili si jambo dogo katika utekelezaji wa mipango ya Serikali, linahitaji ufumbuzi, la sivyo bajeti ya Serikali katika miradi ya maendeleo itaendelea kuwa kiini macho,” amesema Dkt. Ishengoma.
Hata hivyo, amebainisha kuwa upatikanaji wa fedha za ndani za miradi ya maendeleo kwa kipindi cha nusu mwaka zilizokuwa zimetolewa, kilimo kilipangiwa Sh. bilioni 22 lakini mpaka wakati huo zilikuwa hazijatolewa kiasi chochote.

Lusinde amshukia mbunge mwenzie CCM
Dkt. Mpango azitaka kampuni kubwa kuchangamkia fursa