Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeendelea kuwa sehemu inayoenzi mtazamo wa mwanazuioni ‘John Stuart Mill’ kuwa ni soko huru la mawazo (Free Market of Idea) ambapo wabunge wamekuwa wakirusha mawazo yao kwa uhuru na kutaka serikali ‘iyanunue’.

Mbunge wa Geita Vijijini kwa tiketi ya CCM, Joseph Kasheku maarufu kama Msukuma ameitaka serikali kuidhinisha matumizi ya dawa za kulevya aina ya bhangi na mirungi ili kuongeza pato la taifa kwa kupata fedha za kigeni.

Mbunge  wa  Geita vijijini  Joseph Kasheku

Mbunge wa Geita vijijini Joseph Kasheku

Akichangia katika Bunge hilo jana, Mbunge huyo alitetea kuwa bhangi husaidia kuongeza mzuka wa kufanya kazi lakini imezuiwa huku serikali ikiruhusu viroba ambavyo watumiaji wake hushindwa kufanya kazi baada ya kutumia.

“Mheshimiwa mwenyekiti zao la mirungi na bhangi kuna nchi zinaruhusu. Mfano mzuri mfano ni majirani zetu wa Kenya ambao ndege mbili kubwa hutua nchini humo kuchukua mirungi na kupeleka ulaya. Sasa kwa nini sisi tusiendeleze zao hili linalopatikana Geita na maeneo ya Bunda mkoani Mara na maeneo mengine nchini ili wananchi wanufaike kwa kuuza zao hilo ?” Alihoji.

“Kwa wasukuma kule kwetu mtu akitumia bhangi anapata nguvu ya kulima sana hata hekari mbili lakini inakatazwa na wakati huo huo vijana wetu  tumewaruhusu kutumia viroba ambavyo huwadhoofisha sana pengine kushinda hata bhangi, naomba tufanye utafiti upya juu ya hili,” aliendelea.

“Wapo wenzetu humu (wabunge) wanaitumia bhangi na hakuna madhara yoyote, tena wanachangia hoja kwa ufasaha kabisa.”

Hata hivyo, hoja hiyo ilipingwa Serikali, ambapo Naibu Waziri Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto  Dkt Khamis Kigwangalla alieleza kuwa madawa hayo ya kulevya yana madhara makubwa kwa binadamu. Hivyo, Serikali haitaruhusu kwa namna yoyote matumizi yake wala kuyajadili.

 

Tai wapewa mafunzo kuteka ndege zisizo na rubani
Zitto awasha moto ufisadi wa Trilioni 6.8