Serikali nchini imesema Samaki wanaovuliwa kwenda katika masoko mbalimbali wako salamaikiwemo wa kutoka ziwa Victoria na kudai kuwa uvumi unaoenea kuhusu namna kitoweo hicho kinavyohifadhiwa hauna ukweli wowote hivyo wananchi wasiwe na hofu.
Hayo yamebainishwa na Naibu Wazri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega Bungeni jijini Dodoma na kuongeza kuwa samaki wanaovuliwa na kusafirishwa kwenye maeneo mbalimbali nchini ni salama na sio kweli kuwa wanahifadhiwa kwa kutumia dawa za kuhifadhia maiti.
Ulega ambaye alikuwa akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Viti maalum, Cecilia Pareso amesema, “Niwatoe hofu Watanzania, hakuna jambo kama hilo kuwa tuchukue samaki kutoka Mwanza tupeleke Dodoma au Dar es Salaam kwa kuhifadhi na maji ya maiti, halipo jambo la namna hiyo.”
Ameongeza kuwa, “Jambo hili alilolisema Makamu wa Rais ni kwamba watu wana hisia kuwa kipo kitu cha namna hiyo, na aliagiza wizara ya afya ifanye utafiti ili kama ni kweli kinafanyika kitu cha namna hiyo, kizuiwe mara moja.”
Hata hivyo, amesisitiza kuwa samaki wote wanahifadhiwa kwa uangalizi maalum na kwamba sio rahisi kutumia dawa hizo kwenye uhifadhi wa samaki wanaovuliwa kutoka ziwa Victoria.