Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetangaza kuwa michezo ya Ligi Kuu msimu huu na michuano mingine itarejea kuanzia Juni 13.
Afisa Mtendaji Mkuu wa TPLB, Almas Kasongo amesema kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya majadiliano ya baina ya mamlaka za soka na zile za serikali.
“Kwa hiyo baada ya mjadala wa hapa na pale na kupokea taarifa ya kiufundi kutoka kwa kamati ya ufundi, kamati ilijiridhisha kwamba Juni 13 ni muda wa muafaka wa kuendelea na michezo yetu iliyobakia” amesema Kasongo.
“Nichukue fursa hii mimi kama mtendaji mkuu wa bodi ya ligi kutangaza kwamba tarehe ya kurejea kwa ligi ni Juni 13, 2020.”
“Hiki ni kipindi ambacho klabu ziko huru kuanza mazoezi lakini jambo la msingi ni kuzingatia tahadhari zote za virusi vya corona wakati tukisubiri utaratibu na muongozo ambao tutaletewa na kutoka katika kamati ya Corona ya Taifa,” amesema Kasongo.
Kasongo amesema kuwa mbali ya kupanga siku ya kurejea kwa ligi, kamati ya usimamizi na uendeshaji wa ligi imepanga pia kuwa Mei 31 iwe siku ya kutangaza ratiba na utaratibu mzima wa ligi kuchezwa.