Afisa Mtendaji Mkuu wa Fountain Gate Princess Augustine Fulgence amewataka Mashabiki wao watulie wakisubiri kujua usajili mpya wa timu zao, kwa Kuwa time imejipanga vyema.
Fountain Gate Princess yenye maskani yake Jijini Dodoma, msimu wa 2021/2022 uliomalizika May 20 kote Nchini, wameshika nafasi ya pili kwenye mashindano ya Ligi Kuu ya Wanawake baada ya kufikisha alama 54 huku Simba Queens wakitwaa taji hilo.
Amesema bado wanaendelea kukuna vichwa na kufanyia kazi ripoti ya Kocha wao ili msimu wa 2022/2023 warejee kivingine na hatimaye kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake kwa mara ya kwanza.
“Wachezaji wengi tutaendelea nao kwasababu walionesha uwezo mzuri msimu ulioisha lakini pia wana mikataba bado na sisi, lakini wapo ambao tutaachana nao kutokana na sababu mbalimbali lakini ni wachache Sana,” amesema Augustine.
Ameongeza kuwa ili wawe na kikosi imara zaidi msimu ujao na hatimaye kushiriki mashindano ya CECAFA, wanahitaji pia kuongeza baadhi ya wachezaji ambao ni pendekezo la benchi lao la Ufundi na wanaendelea kupambana kuhakikisha wanaitendea haki ripoti hiyo ya sajili mpya.
“Kwa sasa siwezi kukujibu chochote kuhusu usajili mpya kama tumeanza au bado, lakini kama uongozi tutafanyia kazi ripoti ya benchi la ufundi katika maeneo yote ambayo amehitaji tufanye hivyo, tutarejea tukiwa imara zaidi, Mashabiki zetu wakae mkao wa kula,” amesema C E O.