Kocha wa Walinda Lango wa Simba SC Daniel Cadena amesema anajua vitu gani amevibadilisha kwa kipa wake, Ally Salim, ambaye ghafla aligeuka shujaa kwenye mikwaju ya Penati dhidi ya Young Africans juzi Jumapili (Agosti 13), lakini akatoa kitu kuhusu makipa wa timu hiyo.
Akizungumza mjini Morogoro Cadena amesema kuna mafunzo mengi yameanza kumbadilisha kipa huyo na wengine katika kikosi ambayo yatabaki kuwa siri ya kambi.
Cadena alimpongeza Salim akisema kipa huyo ni kijana mdogo na msikivu ambaye baada ya muda atakuja kuwa tegemeo la Simba na timu ya taifa “Taif Stars’.
Kocha huyo aliongeza kuwa mbali na Salim amefurahia viwango vya makipa wengine wa timu hiyo ambao wanaendelea kuishi kama familia na kujiboresha kupitia mazoezi wanayofanya.
“Kwanza nimpongeze Salim. Amefanya kazi nzuri ukiona wakati ule akiwa anadaka penalti na sasa utagundua kuna vitu anaendelea kuboresha. Kuna mengi tunaelekezana kwenye kumjenga ambayo siwezi kuyaweka wazi,” amesema.
“Kitu ambacho mashabiki wa Simba wanatakiwa kujua ni kwamba Simba ina hazina kubwa ya makipa wazuri, sio Salim peke yake hata hawa wengine ni bora sana. Wakati ukifika mtakuja kuwaona.”