Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ limeruhusu wachezaji wa Al Merrikh SC, Ramadan Agab na Bakhit Khamis kucheza mchezo wa mzunguuko wanne wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, hatua ya makundi dhidi ya Simba SC.
Simba SC itakua mwenyeji wa mchezo huo kesho Jumanne (Machi 16), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku ikiongoza msimamo wa kundi A kwa kumiliki alama 07, ikizitangulia AS Vita Club, Al Ahly na Al Merrikh wanaburuza mkia wa kundi hilo.
CAF wametoa ruhusa kwa wachezaji hao wawili kufuatia sintofahamu iliyoibuka saa chache baada ya mchezo wa mzunguuko wa tatu wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, kati ta Al Merrikh dhidi ya Simba uliochezwa mjini Khartoum mwanzoni mwa mwezi huu.
Wachezaji Ramadan Agab na Bakhit Khamis walilalamikiwa na Simba SC kufuatia mashaka ya uhalali wao kutumika kwenye michezo ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, baada ya kufungiwa na chama cha soka nchini Sudan kwa kosa la kusaini katika vilabu viwili kwa wakati mmoja.
Kwa mujibu wa CAF wachezaji hao walifungiwa kucheza mashindano ya ndani lakini hawakatazwi kushiriki Mashindano ya CAF, hivyo wataendelea kuwa wachezjai halali wa Al Merrikh, kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika, msimu huu 2020/21.
Ramadan Agab na Bakhit Khamis wanadaiwa kusaini Al Merrikh na Al Hilal, wakati wa dirisha la usajili mwanzoni mwa msimu huu huko nchini Sudan.