Klabu ya Azam FC itaanzia ugenini katika michuanoya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kucheza dhidi ya Bahir Dar ya Ethiopia, katika mchezo wa Mzunguuko wa Kwanza.
Azam FC ambayo imekuwa ikisaka nafasi ya kutinga hatua ya makundi katika Michuano hiyo ya Afrika, imejiandaa vizuri msimu huu, kufuatia kuwa na kikosi imara ambacho kimejengwa na usajili mkubwa uliofanywa chini ya Kocha Mkuu kutoika Senagal Youssouph Dabo.
Baada ya kupangwa kwa mchezo huo Azam FC kupitia kurasa zake za Mitandao ya Kijamii wameandika: Tumepangwa kucheza dhidi ya Bahir Dar Kenema ya Ethiopia katika raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho la Afrika.
Mchezo wa awali utafanyika kati ya Agosti 18 hadi 20, 2023 ugenini kabla ya mechi ya marudiano kupigwa kati ya Agosti 25 hadi 27, Azam Complex.
Mshindi wa jumla wa mchezo huo, atakutana na Club Africain ya Tunisia, kwenye raundi ya pili na atakayevuka hapo atatinga hatua ya makundi ya michuano hiyo.
Wakati huo huo Klabu ya Singida Big Stars ambayo itashiriki kwa mara ya kwanza Michuano ya CAF, imepangwa kucheza dhidi ya JKU ya Zanzibar.
Mchezo wa mkondo wa kwanza Singida Big Stars itakuwa nyumbani Tanzania Bara, kisha itakwenda Zanzibar kupepetana na wapinzani wao.
Mshindi wa jumla wa mchezo huo atakutana na Future SC ya Misri.
Ikumbukwe kuwa washindi wa michezo ya mzunguuko wa pili hatua ya Kwanza katika Michuano ya Kombe la Shirikisho watakwenda moja kwa moja hatua ya makundi kwa mujibu wa kanuni mpya za michuano hiyo.