Shirikisho la soka Barani Afrika CAF litafanya ukaguzi wa mfumo wa leseni kwa vilabu (Club Licencing) kwenye upande wa miundo mbinu.
CAF watafanya ukaguzi huo wa kutembelea na kutazama miundo mbinu ili kuhakikisha mfumo huo unatekelezeka ipasavyo kwa kuanzia na mtazamo wa vigezo vya miundo mbinu.
Wakati wa miaka kadhaa ya kuzindua mfumo huo wa leseni kwa vilabu ni wazi changamoto kubwa kwenye Bara la Africa imekuwa ni vigezo vya miundo mbinu ambayo kwenye baadhi ya viwanja vinavyotumika wakati wa mashindano imekuwa ikitoa taswira isiyo nzuri kwa mashindano ya CAF.
Kwa mwaka huu 2018 wameandaa ukaguzi kutembelea klabu zote zitakazoshiriki hatua ya makundi kwenye mashindano ya vilabu ya CAF wakijielekeza kwenye kiwango na ubora wa viwanja vya kucheza mechi na viwanja walivyochagua kwa mazoezi.
CAF watachagua kundi la wakaguzi watakaotembelea kwenye klabu za kila mwanachama wake ili kukusanya ripoti itakayowasilishwa na moja kati ya ripoti hiyo ni miundo mbinu ya Uwanja,ripoti itakayothibitisha kama uwanja umefikia kwenye mahitaji ya juu ya kutumika kwa mechi za CAF.
Viwanja ambavyo havitakidhi mahitaji hayo ya juu hautaidhinishwa kutumika kwa mashindano na hautatumika kwa mchezo wowote wa hatua hiyo ya makundi kwa mashindano ya klabu kwa mwaka huu 2018.