Rais wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) Patrice Motsepe amethibitisha kuwa Michuano ya African Super League itaanza kutimua vumbi mwezi Oktoba mwaka huu na kuongeza kwamba kutakuwa na jina jipya kwa ajili ya michuano hiyo ili kuvutia wadhamini zaidi.
Novemba 29, 2019 CAF ilitangaza rasmi kuanzishwa kwa Michuano ya African Super League ikiwa na lengo la kuongeza mapato makubwa ya kifedha yanayotarajiwa kuzidi dola milioni 100 ambazo zitatumika kuboresha miundombinu na kukuza mchezo huo Barani Afrika.
Akizungumzia sababu za michuano hiyo kubadilishwa jina Motsepe amesema baadhi ya Wadhamini wakubwa wamesema historia ya Super League barani Ulaya haikuwa nzuri na kubainisha kuwa jina Super lina maana hasi kwenye soka.
“Tunaweza kubadili jina, lakini kitakachofanyika Oktoba ni uzinduzi tu huku tukiendelea kutumia jina la ‘African Super League’ mpaka pale tutakapolibadili”
Awali michuano hiyo ilipangwa kuhusisha timu 24 katika makundi ya timu nane lakini katika uzinduzi Super League itaanza kwa kundi moja la timu 8 ambazo ni Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini), Al Ahly (Misri), Petro de Luanda (Angola), TP. Mazembe (DR Congo), Horoya (Guinea), Wydad Atheltic Club (Morocco), Simba SC (Tanzania) na Esperance de Tunis (Tunisia).
CAF ilitangaza kuwa mshindi wa michuano hiyo atapata kitita cha dola milioni 11.5 huku kila timu shiriki itatia kibindoni kitita cha Dola za Marekani Milioni 2.5.