Mchezo wa mkondo wa pili wa Ligi Mabingwa Barani Afrika Afrika kati ya Wekundi wa Msimbazi Simba dhidi ya FC Platinum sasa ni rasmi itachezwa saa 11:00 jioni badala ya 1:00 kama ilivyotangazwa awali.
Muda wa kuanza kwa mchezo huo umerudishwa nyuma baada ya uongozi wa klabu ya Simba kuandika barua kwenda Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) kuomba mchezo huo ubadilishwe muda kutokana na jografia ya mji wa Dar es Salaam ilivyo.
Akizungumza na Vyombo vya Habari, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino, Haji Sunday Ramadhan Manara amesema kuwa, baada ya kuandika barua kwenda CAF kuomba mchezo huo kuchezwa saa 11 jioni, Shirikisho hilo limeridhia na kuwapa majibu kuwa sasa mchezo huo utachezwa muda huo badala ya 1:00 usiku.
Amesema kuwa, kilichowasukuma kupeleka maombi hayo ni kutaka mashabiki wengi zaidi kuingia uwanjani kushuhudia mchezo huo kwani nguvu ya wachezaji wao ipo kwa mashabiki ambao siku zote wamekuwa na msukumo wa kikosi chao kupata matokeo mazuri katika uwanja wao wa nyumbani.
“Klabu ya Simba mtaji wake ni mashabiki na ndio mtakaotupa matokeo siku ya mchezo wetu wa marudiano, nguvu ya mashabiki imepelekea klabu zote kubwa za Afrika kushindwa kutamba hivyo ikiwa tutajitokeza kwa wingi, ndani ya dakika 20 tutakuwa tumeshamaliza mchezo.”
“Lakini pia ikiwa tutafuzu basi kizazi hiki cha kina Clatous Chama, Aishi Manula, John Bocco na wengine kitakuwa bora kwani kitakuwa ni kizazi cha kwanza kwenda kufuzu kucheza hatua ya makundi ya Ligi Mabingwa mara ya pili, ni niwahakikishie kwa jinsi morali ilivyo basi ni wazi kazi itakuwa nyepesi kwetu, ” amesema Manara.
Simba SC itatakiwa kushinda mabao mawili kwa sifuri na kuendelea ili kujihakikishia safari ya kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu, huku FC Platnum wakihitaji sare ama ushindi kufikia lengo la kuwatupa nje Mabingwa hao wa Tanzania Bara.
Timu yoyote inayotinga hatua hiyo ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, inakuwa imejihakikishia kitita cha Dola 550,000 (zaidi ya Sh 1.2 bilioni), kiasi ambacho kinaweza kuongezeka ikiwa itasonga mbele katika hatua zinazofuata.