Klabu ya Namungo FC, ipo kwenye hatua za kujihakikishia kupata dola 275,000 (zaidi ya Sh milioni 635 za Tanzania) kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kama zawadi.
Fedha hizo zitatolewa kwa Namungo FC endapo itafanikiwa kutinga hatua ya makundi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo hivi sasa inasubiri mchezo wa mkondo wa pili dhidi ya CD Primeiro de Agosto utakayochezwa leo Alhamisi kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi.
Fedha hizo hutotolewa na CAF kwa kila timu ambayo imefanikiwa kufika kwenye hatua ya makundi. Namungo ikitinga makundi, itakuwa Kundi D na timu za Nkana, Raja Club Athletic na Pyramids.
Wakati Namungo FC wakisubiri kitita hicho cha pesa, Afisa Mtendaji Mkuu ‘CEO’ wa Namungo FC Omar Kaaya na Wachezaji wa Namungo Fred Tangalo, Lucas Kikoti na Khamis Fakhi waliokuwa wamekwama mjini Luanda, Angola wanatarajiwa kurejea nchini Jumamosi ama Jumatatu.
Kaaya na wachezaji hao wanne aliwekwa Karantini nchini Angola baada ya kukutwa na maambuziki ya Virusi vya Korona, saa chache baada ya kikosi cha Namungo FC kuwasili mjini Luanda majuma mawili yaliyopita kwa ajili ya mchezo wa hatua ya 32 Bora dhidi ya CD Primeiro de Agosto.
Jana mchana ilithibitika Kaaya na wenzake wametolewa karantini kwa kutuma video nchini kwa njia ya mitandao ya kijamii, na taarifa zinaeleza kuwa kwa sasa wapo nyumbani kwa Balozi Mziray.
Hata hivyo bado haijafahamika kama Kaaya na wenzake watarejea nchini kwa gharama za Serikali ya Angola, ama gharama za Namungo FC.