Kocha Mkuu wa Simba SC, Robert Oliveira Robertinho’, amesema mipango yake ni kuona Simba SC inafanya vizuri kwenye michuano ya Kimataifa na sasa anaumiza kichwa kuona namna gani anakiandaa kikosi chake kwa ajili ya michuano hiyo.
Robertinho ambaye kwa sasa yupo mapumzikoni nchini kwao Brazil, amesema anataka kuona Simba SC inafanya vizuri msimu ujao hasa kwenye mashindano ya Kimataifa na tayari ameshakabidhi ripoti yake na wachezaji anaowataka kwenye timu yake kuweza kufanya vizuri michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika watakayoshiriki.
“Unajua hatukuwa na msimu mzuri kwa sababu hatukuweza kuchukua ubingwa wowote na hayakuwa malengo yetu, tunahitaji kuona tunaenda mbali zaidi msimu ujao kupitia wachezaji ambao nahitaji kuwanao, nimeshwaambia viongozi wachezaji wanaotakiwa ndani ya Simba SC,” amesema Robertinho.
Amesema ili kufika mbali kwenye mashindano ya Kimataifa wanahitaji wachezaji wanaoweza kupambana na timu kubwa na kupata matokeo mazuri.
“Kwangu kazi nimemaliza, nimeshawapa ripoti yangu viongozi, kwa sasa kazi ipo kwa viongozi kuwapata wachezaji wote niliowaagiza viongozi wangu, naamini tutawapata na baada ya hapo kazi itakuwa kwangu na wachezaji wangu,” amesema Robertinho na kuongeza;
“Simba SC ina jina kubwa Afrika kwa sasa, hivyo ni lazima tuwe na wachezaji wenye sifa hizo, wachezaji ambao wanaweza kukupa matokeo kwenye mechi yoyote, nikiwapata hao niliowaomba viongozi na wengine ambao ninao, tunaweza tukafanya vizuri msimu ujao na kurejesha furaha ya mashabiki wetu,” amesema Robertinho.
Amesema Simba SC msimu huu itaanza kushiriki michuano ya ‘Super League’ inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ hivyo lazima wawe na wachezaji watakaopambana na timu kubwa kama Al Ahly na Mamelod Sundown ambazo zote zitakuwapo kwenye michuano hiyo itakayohusisha timu nane.
Katika hatua nyingine, Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema wanafahamu maumivu wanayopitia Mashabiki na Wanachama wa Simba SC hasa kutokana na kelele za watani zao Young Africans ambao wameshinda Taji la Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.
Ahmed amesema kelele hizo za watani zao ni chachu kwao kujipanga kwa ajili ya kufanya vizuri msimu ujao kwenye michuano ya ndani na ile ya Kimataifa.
“Kiujumla kama timu hatuna cha kujivunia sana maana hatujapata tulichokihitaji msimu huu, hii inatupa nafasi ya kujipanga zaidi kwa msimu ujao, kwani ubingwa unahitaji wachezaji bora na timu imara ni jukumu letu viongozi kutafuta wachezaji sahihi na kutengeneza timu madhubuti, hilo limeshaanza kufanyika kwa umaridadi wa hali ya juu sana, hizi kelele za upunde wa pili tutazijibu msimu ujao.” amesema Ahmed Ally.