Boniface Gideon – Tanga.
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali – CAG, Mkoa wa Tanga amebaini uwepo wa dosari namna ya uendeshaji wa miradi ya masoko ya Samaki huku miradi hiyo ikishindwa kutoa faida licha ya kuonekana Serikali kuwekeza fedha nyingi kupitia sekta hiyo ya Uvuvi.
Aidha Halmashauri hiyo imeonekana kupunguza kiwango cha hoja zilizoibuliwa na CAG kwa Mwaka wa fedha 2021/2022 kutoka hoja 44 hadi kufikia hoja 41 huku hoja nyingi zikionekana kujirudia kila mwaka hali iliyoonekana kuwakasirisha viongozi wengi wa Halmashauri hiyo hususani Madiwani na Mkuu wa Mkoa huo Waziri Kindamba.
Hoja hizo za CAG zimeibuliwa wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani kilichoketi kujadili Ripoti ya CAG, katika kikao kiliongozwa na Mwenyekiti wake ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba na kuchambua hoja 41 ambazo CAG amezitolea kwenye Ripoti yake ya mwaka wa fedha 2021/2022 na zinatakiwa zifanyiwe kazi kabla ya mwaka wa fedha kufungwa juni 30 mwaka huu.
CAG, ameonesha kutokuridhishwa na namna Halmashauri hiyo inavyoendesha na kusimamia Masoko ya Samaki huku Mapato yatokanayo na Sekta ya Uvuvi yakionekana kupotea kutokana na isimamizi mbovu, Masoko hayo ni Mchukuuni,Tongoni na Deepsea huku soko kuu la Samaki Kisosora likinyooshewa vidole na Madiwani kufanyiwa ukarabati na ili kudhibiti upotevu wa mapato.
Akijibu hoja hiyo, Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Spora Liana alisema, ‘’tumetenga mil.300 kwaajili ya ukarabati na ujenzi wa vizimba vya kuuzia Samaki soko la Deepsea, kuhusu Masoko mengine ya Tongoni na Mchukuuni yapo kwenye mradi wa Botnar foundation lakini pia wavuvi tuliwanunulia Boti kwaajili ya kuwahamasisha kuanza kufanya kazi ya uvuvi.’’
Hata hivyo hoja hiyo ilimkasirisisha Mkuu wa Mkoa ambapo alisema jiji la Tanga ni kioo cha Mkoa huo na Mikoa ya Kanda ya Kaskazini Mashariki, kwani ina ukanda mzuri wa Bahari uwepo wa Samaki wengi wa aina mbalimbali ambao hawapatikani huko katika mikoa ya Bara.
“Mkurugenzi hakikisha unawapeleka Wataalamu wako hata huko Pemba waende wakajifunze uchumi wa Bluu ili tuende sawa kwapamoja, tunahitaji uchumi wetu ukue hasa kupitia Bahari yetu ambayo wengine wanaililia,‘’ alisema Waziri Kindamba
Miradi mingine ambayo CAG ameitilia shaka ni Kuchelewa ujenzi wa jengo la Stendi mabasi kange, mfumo mbovu wa ukusanyaji mapato eneo mapumziko forodhani ,Fremu za maduka ya Biashara za Stendi ya Pongwe ambayo inafremu za maduka 88 lakini mfumo wa mapato hauonyeshi kulipiwa.
Kwa mujibu wa Ofisa Biashara wa Halmashauri hiyo, Lusia Malando ni Shilingi 400,000 kati ya milioni 3 pekee ndizo zimelipiwa kinyume na makubaliano kati ya Wafanyabiashara na Halmashauri kutokana na kuwa Fremu hizo hazikujengwa na Halmashauri bali Wafanyabiashara kwa makubaliano maalumu.