Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imebaini uwepo wa uozo wa ubadhirifu wa fedha katika hospitali ya Umma ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Ripoti hiyo ya Mwaka wa Fedha 2016/17 imebaini kuwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, baadhi ya wagonjwa wenye bima za afya walilipishwa pia fedha taslimu, kinyume cha taratibu.
Kutokana na ubadhirifu wa fedha uliobainika ukifanywa na wafanyakazi wa hospitali hiyo, makampuni ya bima ya afya yalikataa kulipia gharama za matibabu ya sh.1.86 bilioni.
Aidha, imebainisha kuwa sh241.97 milioni zililipwa katika Hosptali hiyo kama gharama za dawa lakini dawa hizo hazikuwafikia wagonjwa husika.
“Katika Mwaka huo wa fedha, nilibaini kuwa kiasi cha sh.1.86 bilioni zilizoanishwa kama gharama za bili ya matibabu ya wagonjwa wenye bima zilikataliwa na makampuni ya bima. Baadhi ya maafisa walihusika katika ubadhirifu huo,” alisema CAG, Prof. Mussa Asaad katika ripoti hiyo.
Profesa Assad alihoji ubadhirifu huo unaofanyika katika hospitali za umma na kuongeza kuwa chanzo chake ni usimamizi na ufuatiliaji mbovu ambao unaweza kusababisha hasara kubwa kwa hospitali nyingi za umma.
CAG ameitaka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kufanya uchunguzi juu ya bili zilizokataliwa na makampuni ya bima za afya na kuchukua hatua stahiki dhidi ya waliosababisha hasara hiyo.